Mwandishi afungwa kwa kushiriki ngono nje ya ndoa

Mwandishi wa habari wa Morocco amehukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela kwa kosa la kufanya ngono kabla ya ndoa na kutoa mimba hiyo.

Wanaharakati wanasema kuwa hiyo ni moja ya mbinu ya kuwadhoofisha waandishi wakosoaji.

Hajar Raissouni alikamatwa na mchumba wake wakati wakiwa wanatoka kliniki iliyopo mji mkuu wa Rabat mwezi Agosti.

Mtuhumiwa huyo mwenye miaka 28 alikanusha madai yanayomkabili na kusema kuwa alienda hospitalini kwa ajili ya matibabu ya damu iliyokuwa inatoka kwa ndani.

Bi.Raissouni anafanya kazi katika gazeti binafsi ambalo huwa linakosoa serikali.

Mwandishi huyo wa gazeti la Akhbar Al-Yaoum daily , anasema kuwa anakataa kesi hiyo dhidi yake na kudai kuwa ni kesi ya kisiasa, amesema pia amekuwa akihojiwa na polisi kuhusu familia yake na uandishi wake.

Akiwa amevaa kitambaa cheusi kichwani , bi .Raissouni alifika mahakamani akiwa mtulivu .

Yeye na mchumba wake ambaye ni raia wa Sudan walikanusha kutoa mimba.

" Tumeshtushwa na haya madai," wakili wake alisema, Abdelmoula El Marouri, aliiambia Reuters kuwa rekodi zote za matibabu na ushaidi uliotolewa kisheria unapaswa kulenga kuwa hana hatia.

Ingawa anasema kuwa atakata rufaa dhidi ya kesi hiyo.

Mwendesha mashtaka wa kesi hiyo anasema kuwa sababu zilizopelekea mwandishi huyo kukamatwa hazina uhusiano wowote na kazi yake kama mwandishi na kliniki aliyoenda ilikuwa chini ya uangalizi wa polisi ili kukamata watu wanaotoa mimba kinyume na sheria.

Mahakama imemuhukumu mwaka mmoja na daktari aliyetoa mimba hiyo alihukumiwa miaka miwili.

Daktari msaidizi na nesi wa kliniki hiyo walikutwa hawana hatia ingawa walipewa angalizo.

Ahmed Benchemsi, kutoka Human Rights Watch,ameelezea kesi hiyo kuwa haikuzingatia haki za binadamu na imeingilia uhuru wa mtu binafsi.

-BBC