Mwandishi wa habari atiwa mbaroni nchini Tanzania

ECoIMLfU8AA_sjK
ECoIMLfU8AA_sjK

Polisi nchini Tanzania wanamshikilia mwanahabari Joseph Gandye kwa madai ya kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni.

Gandye, ambaye ni mhariri na uzalishaji maudhui na msimamizi msaidizi wa Watetezi TV amekamatwa jana mchana kwa madai ya kuchapisha taarifa za uongo kuhusu ukatili wa polisi wa kituo cha Mafinga, Iringa.

 Kwa mujibu wa mtandao wa kijamii wa Twitter wa Watetezi TV, Gandye amesafirishwa alfajiri ya leo kwenda Iringa ili kukabiliana na tuhuma hizo.

Watetezi TV inamilikiwa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binaadamu Tanzania (THRDC) na imejikita zaidi kwenye taarifa za ukiukwaji wa haki za binaadamu nchini humo.

Kwa mujibu wa Mratibu wa Kitaifa wa THRDC, taarifa iliyomtia matatani Gondye inahusu tuhuma za polisi mkoani Iringa kuwalazimisha mahabusu kulawitiana katika kituo cha Mafinga.

Mahabusu hao sita walikuwa wanakabiliwa na tuhuma za kumuibia mwajiri wao na wanadaiwa kupigwa pia na polisi.

"Juni 17, waandishi wa Watetezi TV walipokea ripoti za matendo hayo ya kudhalilisha katika kituo cha polisi Mafinga, mkoani Iringa. Baada ya kupokea taarifa, Joseph Gandye alisafiri kwenda Iringa na kufanya uchunguzi wa kina kisha kuchapisha taarifa hiyo kwenye mitandao (ya Watetezi TV) ya Facebook, Twitter na You Tube," inaeleza taarifa kutoka THRDC.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa alipinga vikali taarifa hiyo Agosti 14 na kutoa onyo kali dhidi ya kupakwa matope kwa jeshi la polisi na maafisa wake.

Kamati ya kimataifa ya kutetea waandishi wa habari (CPJ) umeonesha mashaka yake juu ya kukamatwa kwa mwanahabari huyo.

Kukamatwa kwa Gondye kuna kuja wiki chache baada ya mwandishi wa uchunguzi Erick Kabendera kupandishwa kizimbani kwa mashtaka ya ubadhirifu wa kiuchumi.

Kumekuwa na wasiwasi ndani na nje ya Tanzania kuhusu namna ambavyo Kabendera alikamatwa, na taswira inayotokana na hatua hiyo kwa uhuru wa yombo vya habari nchini humo.

Kabendera anatuhumiwa na kujihusisha na genge la uhalifu na uhujumu wa uchumi nchini Tanzania, shtaka la pili ni la kukwepa kulipa kodi ya zaidi ya milioni mia moja sabini za kitanzania.

Kosa la tatu ni la utakatishaji fedha zenye thamani ya zaidi ya millioni mia moja na sabini.

Awali maafisa wa polisi na wale wa idara ya uhamiaji walisema anachunguzwa kuhusu utata wa uraia wake. Baadaye mawakili wake walitoa taarifa wakieleza mteja wao atashtakiwa kwa kuhusika na ripoti iliyochapiswha katika jarida la The Economist, lakini mahakamani kibao kikageuka tena na kuwa kesi ya ubadhirifu wa kiuchumi.