Mwili wa mwanamke wapatikana ndani ya gari, macho yang'olewa

Mwili wa mwanamke umepatikana ukiwa ndani mwa gari katika soko la Mwingi, Jumatatu.

Msimamizi wa kaunti ndogo ya Mwingi ya kati Alex Mutemi alisema kwamba mwanamke huyo alitambuliwa kama Eunice Kiema kutoka Kyuso, Mwingi Kaskazini.

Hata hivyo, alisema kwamba alizaliwa Mui, Mwingi kati.

''Tuliamkia taarifa za kuhuzunisha asubuhi ya leo kwa kumpoteza kupitia mauaji ya kikatili mkufunzi wetu ambaye ni afisa wa kliniki anayesomea katika chuo cha KMTC, Mwingi.

Macho yake yaling'olewa, sehemu ya miguu yake kuchomwa huku akiwa na majeraha ya kudungwa kisu.

Hatimaye, mwili wake ulipelekwa katika makavani. Kamanda wa polisi wa Mwingi kati Peter Mutuma alisema kwamba kikosi chake pamoja na maafisa wa DCI wameanzisha uchunguzi.

"Mshukiwa alikuwa na malengo ya kuchoma gari hilo aina ya Toyota Raum, nambari ya usajili KCJ, 451B, rangi ya kijivu. Kiberiti kilipatikana karibu na tukio hilo." Mutuma alisema.

Wakaazi waliwahimiza polisi kuimarisha hali ya usalama katika mji mwa Mwingi.

Mkaazi Ndanu Kimanzi alisema ni aibu sana kupoteza maisha kwa wauaji katili, huku akiomba polisi wapige doria mchana na usiku.

"Ni masikitiko makubwa sana mwanamke kuuliwa kinyama, ilhali tunao maafisa wa polisi Mwingi. Tunataka watuhakikishie hali shwari ya usalama," alisema huku akitokwa na machozi.

Mkaazi mwingine aliyejitambulisha kama Ras alitoa wito wa kuongezwa kwa maafisa wa polisi.

Alisema kwamba Mwingi kumekuwa na usalama na hakuna anayepewa nafasi kuleta hofu. Aliwarai wakaazi kushirikiana na polisi kuleta amani na utulivu.