MAGUFLI

Tanzania na Kenya zarushiana makonde ya kidiplomasia, KQ hairuhusiwi Tanzania

Siku moja baada ya Kenya kutoijumuisha Tanzania katika orodha ya nchi ambazo ndege zake zitaruhusiwa kuingia nchini Kenya, Tanzania imepiga marufuku ndege za shirika la Kenya Airways kuingia nchini humo.

katika barua kwa Kenya Airways, mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya shughuli za ndege nchini Tanzania Hamza Johari alisema kwamba waliafikia uamuzi kufutilia mbali idhini ya ndege za KQ kuingia nchini humo.

Alisema kwamba Tanzania imetamaushwa na hatua ya Kenya kuifungia nje ya nchi ambazo zinaruhusiwa nchini Kenya wakati safari za ndege za kimatifa zinaporejea nchini Kenya.

kq-pic

Johari alisema kwamba barua hii mpya inafuta maafikiano yote ya awali yaliokuwa yameipa KQ idhini kuingia nchini humo ikiwemo barua ya Julai 30, 2020.

Kulingana na waziri wa uchukuzi James Macharia nchi zilizopewa idhini kuingia Kenya ni Uchina, Korea Kusini, Japan, Canada, Zimbabwe na Ethiopia. Nchi zingine zilizoruhusiwa ni Ufaransa, Rwanda, Uganda, Namibia na Morroco.

Waziri Macharia alisema nchi zilizopewa idhini zimesajili kupungua kwa maambukizi ya virusi vya corona. Alisema orodha hiyo itafanyiwa mabadiliko kila mara kulingana na hali itakavyokuwa na utathmini wa usambaaji wa virusi vya corona kote duniani.

Tanzania imelaumiwa kwa kuficha takwimu kuhusu maambukizi ya virusi vya corona. Mara ya mwisho nchi hiyo kutangaza deta za maambukizi ya covid-19 ilikuwa Aprili 29, ambapo jumla ya watu 480 walikuwa wameambukizwa na 21 kufariki.

magufuli uhuru

Siku ya Jumatatu rais Uhuru Kenyatta aliwatawahadharisha wakenya dhidi ya maeneo ambayo yamekataa kuwaeleza wananchi wake ukweli kuhusu maambukizi ya corona na hata kuwekea vyombo vya habari vikwazo dhidi ya kutangaza taarifa kuhusiana na janga la covid-19.

“Tusijilinganishe na kusema kwamba baadhi ya maeneo hayana virusi. Mbona tuko nayo na wao hawana? Wacha niwakumbushe wakenya, tunaishi katika demokrasia, ambapo kuna uhuru wa vyombo vya habari. Kama taifa hatuna uwezo wa kuficha kitu chochote, kinachofanyika tunawaambia,” Uhuru alisema.

Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli amekuwa akisema kwamba nchi yake tayari imeshinda virusi vya corona kwa uwezo wake Mungu na kushauri wananchi wake kuendelea na shughuli zao bila tashwishi.

Photo Credits: Hisani

Read More:

Comments

comments