Akizungumza na KTN, Badi amesema kundi lake limefaulu kuchimba visima 93 katika siku 100 zilizopita. Badi amesema kupitia mpango huo, maji yatakuwa yakipelekwa kwa wakaazi wa jiji bure bila malipo katika mitaa ya mabanda.
Ameongeza kwamba eneo la katikati mwa jiji linafanyiwa mageuzi ndio kwa sababu kuna mrundiko wa taka kwa ajili kuna kazi zinazoendelea kutekelezwa kwa miezi 3 hadi 6 ijayo.
Ameongeza kwamba mamlaka hiyo hailengi kutwaa mipango ya gavana Sonko bali itaunganisha mipango hiyo ili itekelezwe kwa manufaa ya wakaazi wa Nairobi.
Badi amesema wana mpango wa kumaliza tatizo la uhaba wa maji jijini.
"Tumekuwa na makundi ambayo yanahujumu juhudi za serikali ya kaunti kutoa huduma kama maji, umeme na miundo msingi. Sasa tupo katika harakati za kusajili wauzaji wote wa maji ili tujue wanayatoa wapi maji na wapi wanayasambaza’ amesema Badi.
Siku ya Jumatatu, Badi alisimamisha ujenzi wa jumba moja la mstawishaji wa kibinafsi katika eneo la Parkland ambapo aliandamana na mwakilishi wadi wa eneo hilo Jayendra Malde na mbunge wa Westlands Timothy Wanyonyi na kipande hicho cha ardhi kilichokuwa kimenyakuliwa sasa kitatumiwa kujenga kituo cha afya kuwasaidia wenyeji.