Makali ya KOT yamewashangaza hata watumiaji wengine wa mitandao ya kijamii na ingawaje wengi huchukulia baadhi ya yanayochapishwa katika KOT kama burudani au mzaha, mengine sio mazuri yanayofaa kusifiwa kwa sababu yanawaathiri watu ambao wana hisia na wanaokwaza zaidi ya mara moja na mambo yanayoandikwa katika mitandao .
Hata hivyo, baadhi ya vinavyochapishwa na KOT vinazua maswali ya je, mambo hayo hupatikanaje? Unafaa kuwa muangalifu kuhusu maisha yako na unaowaambia kuhusu kila hatua yako kwa sababu KOT sio Aliens ni watu kama mimi na wewe walio na muda wa kutosha, bundles za kuharibu na makovu yasiojulikana na hivyo basi mtandao unawapa fursa bora ya kujiona wapo juu yako kwa kuyageuza maisha yako juu chini . Inakuaje baadhi ya vitu vya siri kabisa, vya ndani wakati mwingine vinapatikana mitandaoni? Ni kwa sababu baadhi ya watu unaowaamini wana akaunti feki za kumbi za kijamii na wanazitumia kutoa siri kama hizo ama wanasambaza siri zako ambazo badala yake hulipa jeshi kama KOT mambo ya kutosha kulipua kila unachopenda maishani mwako .
Nguvu na ustadi wa jeshi la KOT zinafaa kutumiwa vizuri kupigania masuala yanayowaathiri wakenya na kuwafanya viongozi wa kisiasa na taasisi za umma kuwajibika . KOT inafaa kuanza kutumia uwezo wake kuleta machoni na katika mijadala masuala kama jinsi kodi yetu inavyotumiwa vibaya na ingawaje baadhi ya mambo ambayo wameweza kuyashughulikia hapo awali yanaweza kusifika kwa kuwashambulia watu waliostahili hasa wachokozi wenzao katika mataifa mengine kama vile vita vya mitandao vya mara kwa mara dhidi ya Nigeria, Uganda , Tanzania na hata Afrika Kusini. KOT inafaa kuepuka kuingiza masuala ya kibinafsi ya watu hasa walio mashuhuri kwa sababu vitu kama hivyo havijengi ila vinabomoa .
Macelebs na watu wengine wa kawaida ambao hushambuliwa na KOT ni watu kama mimi na wewe na baadhi ya ukatili ambao huelekezewa haufai kabisa. KOT inafaa kutafuta mbinu za kutumia raslimali zilizopo kama uwepo wa mtandao na uhuru wa kutumia kumbi hizo kwa mambo yanayoleta manufaa ya jumla kwa wote bali sio mambo kama kuwashambulia, kuwatusi na kuwafanyia kejeli watu kwa sababu ya madai ya kusema hivi au kufanya vile . Kwa mfano mwanahabari Yvonne Okwara amejipata akipondwa sana na KOT kwa sababu ya msimamo wake kuhusu hatua ya baadhi ya watumizi wa mitandao kusambaza picha za utupu za Brenda Cherotich ambaye alipona virusi vya Corona. Yvyonne alikuwa na haki ya kutoa maoni yake bila kuhofia adhabu ya kupigwa vijembe na kuchomwa wazi katika grili ya KOT .
Utumiaji mbaya wa fursa za kuwepo uhuru na uwazi katika matumizi ya mitandao ndiko kunazozifanya baadhi ya serikali kubana matumzi ya mitandao miongoni mwa wananchi wao , na tusije tukailazimu serikali zetu Afrika kuanza kubana utumizi na uhuru wa mitandao kwa ajili ya ukosefu wa kutowajibika kwa baadhi yetu na hasa jeshi lisilo na sura kama vile KOT .