What Next? Maelfu wapoteza kazi na kipato kwa ajili ya coronavirus. Soma kuhusu taaluma zilizoathiriwa zaidi

Mwezi Disemba mwaka wa 2019 wakati  visa vya virusi vya corona vilipoanza kuripotiwa nchini China, hakuna aliyejua kwamba wakati utafika kwa ugonjwa huo kuathiri maisha yake kwa undani na moja kwa moja. Wengi walifahamu tu kwamba ugonjwa huo ungeweza kuthibitiwa huko China na hata mataifa mengi yalijipata katika janga la kiafya baada ya mkurupuko wa virusi hivyo .

Humu nchini, hatua ya serikali kutangaza marufuku za watu kusafiri kwenda sehemu moja hadi nyingine na hata kusitisha safari za ndege kimataifa imezua athari mbalimbali na kuna wafanyikazi wengi ambao wamepoteza kazi zao na wengine  maelfu waliolazimika kukubali kupunguzwa kwa malipo yao kwa sababu ya hali ngumu ya kiuchumi iliyosababishwa na ugonjwa wa corona. Kando na kuathiriwa kwa maisha kwa njia ya kijamii kwa kuzuiwa kwenda sehemu kama vile makanisani na misikitini, wakenya pia wamelazimika kuzoea maisha bila kutoka nyumbani kwenda kutembea. Baadhi ya wafanyikazi walioathiriwa pakubwa na janga la corona ni;

 Walimu  wa shule za kibinafsi

Walimu wa shule za kibinafsi wamejipata katika hali mbaya hasa baada ya shule kufungwa na hivyo basi kuwa vigumu kwa wazazi kulipa karo ambayo ndio ada inayotumiwa kuwalipa mishahara. Kuna hofu kwamba shule nyingi za kibinafsi huenda zikalazimika kufungwa kwa ajili ya kutokuwa na fedh za kuendesha oparesheni zake na kuwalipa walimu na wafanyikazi wengine. Julius Kadima na mkewe wote ni walimu wa shule moja ya kibinafsi jijini na wamekuwa wakifikiria kuhusu hatua watakayochukua pindi maisha yanaporejea hali ya kawaida kwani hawajalipwa mishahara ya miezi ya Aprili, Mei na Juni. Mwajiri wao  amewaarifu kwamba itakuwa vigumu wao kulipwa ilhali wanafunzi wote wapo nyumbani. Jitihada zao za kutaka kupokea angalau kiasi kidogo cha fedha za matumizi ya nyumbani kwa ajili ya huduma za mafunzo ya mtandao waliotoa katika siku za mwanzo mwanzo zimeambulia patupu kwani hakuna mzazi aliye tayari kulipa karo kwa masomo yaliyotolewa na walimu kupitia mtandaoni.

  Wafanyikazi wa hoteli, baa maneo ya burudani  na sekta ya Utalii

Iwapo kuna sekta ambayo imeathiriwa sana na janga la corona basi ni sekta ya hoteli na  utalii. Hoteli nyingi zilifungwa pindi tu janga la corona lilipozidi ili kuzuia watu wengi kutangamana katika sehemu moja na hivyo basi kufanya kuwa vigumu kwa hoteli kuendelea kuhudumu. Hoteli nyingi zililazimika kuwafuta  kazi wafanyikazi kwa sababu hapakuwa na njia ya kutafuta  pesa za kuliwapa. Wengi walilazimika kurejea nyumbani na wakati huu wanapitia wakati mgumu kumudu maisha yao mijini  kwa sababu wengi wanahitajika kulipa kodi na hata  kununua  chakula. Utalii nao ulivurugwa pindi tu serikali ilipotangaza marufuku ya safari za ndege za kutoka na kuingia nchini. Wafanyikazi wengi wanaonufaika na mapato ya utalii wamejipata bila kazi kwa kipindi hicho kizima na wadadisi wanasema huenda ikachukua muda mrefu kwa utalii kufufuliwa kwani italazimu virusi hivyo kuangamizwa kabisa kabla ya raia yeyote wa kigeni kuwa na imani ya kutaka kuja nchini.

Wafanyikazi wa  mashirika ya safari za ndege  

Sekta ya usafiri wa ndege imevurugwa kabisa na janga la corona kwa sababu  kampuni nyingi za ndege zilisitisha oparesheni pindi tu nchi mbalimbali zilipoanza kupiga marufuku safari za ndege. Ni ndege za kusafirisha mizigo pekee ndizo zilizoruhusiwa kuendelea na shughuli. Hatua hiyo ya kutoweza kufanya kazi kwa muda huo wote imetia hatarini nafasi za kazi  za maelfu ya wahudumu katika sekta hiyo  ambao wengi waliachiliwa na waajiri wao kurejea nyumbani na kwa sasa kampuni nyingi zinaendelea kuwapunguza wafanyikazi wake kabla ya anga kufunguliwa kwa shughuli za usafiri.

 Waagizaji wa bidhaa kutoka nje

Wafanyibiashara wanaogiza bidhaa zao kutoka nje na hasa China wamejipata mashakani kwani wengi wao wamelazimika kusitisha biashara zao. Hali nchini ilikuwa mbaya wakati wafanyikazi wengi wa bandari walipoambukizwa virusi vya corona na kulemaza utaratibu wa kuachilia mizigo bandarini kusafirishwa katika sehemu nyingi za taifa. Kwa sasa tatizo hilo pia limeanza kuwakumba madreva wa matrela wanaosafirisha bidhaa hizo kutoka bandari hadi mataifa jirani.

 Wasanii

Kwa sababu ya kupigwa  marufuku kwa mikusanyiko ya watu, wasanii na watumbuizaji wengine wamelazimika kutafuta njia nyingine za kujipa kipato wakiwa nyumbani. Imekuwa vigumu kwa watu kulipia tamasha za muziki ambazo hawawezi kuhudhuria na hafla zilizokuwa zimeratibiwa kuandaliwa nazo zilifutiliwa mbali pindi baada ya janga la corona kusambaa .