Ni kubaya! Ruto anyolewa baada ya mgao wa bajeti yake kupunguzwa kwa asilimia 40

Bajeti ya afisi ya  naibu wa rais William Ruto imepunguzwa kwa takriban asilimia 40 katika kinachoonekana kama kuendelea kwa kampeini ya kumpunguza makali kisiasa.

Mgao wa bajeti yake sasa umepunguzwa hadi shilingi bilioni 1.4 kutoka shilingi bilioni 2.4 hatua ambayo sasa itamnyima fedha za walipa ushuru ili kuweza kufanya ziara za kwenda sehemu mbalimbali za nchi. Ingawaje siye peke yake  kuathiriwa na mkato huo wa bajeti, afisi yake  ni miongoni mwa zilizoathiriwa zaidi na kupunguzwa kwa migao. Bajeti ya masuala ya baraza la mawaziri imepunguzwa kwa asilimia 21 baada ya kutengewa shilingi bilioni 2.2 kutoka kiasi cha awali cha shilingi bilioni 2.8.  Bajeti ya masuala ya Ikulu  ambayo inasheheni afisi ya rais  itapokea shilingi bilioni 3.8  kutoka shilingi bilioni 5.4 . Afisi ya rais imedondoa baadhi ya nafasi na vitengo hatua inayoeleza kupungua kwa  bajeti yake.

Baadhi ya vitengo vinavyohitaji ufadhili katika afisi ya Ruto vimepunguzwa fedha hadi kwa asilimia zaidi ya 80. Ruto sasa atakuwa na shilingi milioni 96.8 za kusafiri humu nchini  kutoka shilingi milioni 193.6 mwaka huu wa kifedha . Mgao huo mkubwa wa fedha za kusafiri ulimwezesha yeye na washirika wake kufanya ziara za kila mara nchini hatua iliyowafanya kupewa  jina la  ‘tanga tang’ baada ya kutumia fursa hiyo kuanza kufanya kampeini za urais ili kumrithi rais Uhuru Kenyatta.

Mgao wake wa bajeti ya usafiri nje ya nchi umepunguzwa kwa zaidi ya asilimia 60  hadi shilingi  milioni 33.6 kutoka kiasi cha awali cha shilingi milioni 89.6. Bajeti yake ya kuwaburudisha wageni wake  ndio iliyopunguzwa kwa kiasi kikubwa  cha zaidi ya asilimia 87 kutoka shilingi  milioni 197.9 hadi shilingi milioni 23.9 . Bajeti ya kununua mafuta ya petrol katika afisi ya Ruto pia imepunguzwa  hadi shilingi  milioni 14.2 kutoka shilingi milioni 28.4  ilhali gharama nyingine za oparesheni zilipunguzwa kwa asilimia 66 kutoka shilingi milioni  307.3  hadi shilingi milioni 103.6

Kwa upande mwingine serikali imetoa mgao wa bajeti kwa  mwaka mzima wa kifedha kwa afisi ya aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga na  afisi za marais wa zamani na makamu wa rais wa zamani. Katika mwaka mpya wa kifedha hazina ya kitaifa imeitengea afisi ya  Odinga shilingi milioni 71.9 . mwaka jana bajeti yake ilipuguzwa katika bajeti ya ziada.

Katika bajeti mpya  Odinga atapokea shilingi milioni 10 za kuwalipa wafanyikazi wasio wa kudumu pia atapokea shilingi milioni 20  za kugharamia huduma za bima, shilingi milioni 26 kununua magari mapya na shilingi milioni 10 za kununua fanicha. Hatua hiyo sasa itafikisha kikomo  malumbano ya muda mrefu  yaliyopelekea afisi yake kunyimwa fedha  kwa madai kwamba alikuwa bado katika siasa  na hakuwa amestaafu. Pia ni ishara ya kuboreka kwa uhusiano wake na rais Kenyatta tangu walipotia saini mwafaka wa handshake  na  juhudi za BBI