Danganya toto:‘Sikusoma mkataba wa kuhamisha majukumu ya Jiji kwa serikali kuu.’ - Sonko asema

Sonko
Sonko
Gavana wa Nairobi Mike Sonko sasa amedai kuna makundi ya watu ‘wahalifu’ ambao wameteka mchakato wa kuhamisha majukumu kutoka kwa kaunti ya jiji hadi kwa serikali kuu  baada yake kusaini mkataba wa kufanya hivyo mwezi februari.

Sonko siku ya Jumatano, alitishia kuukatiza mkataba huo. Amesema atawasilisha kesi kortini ili kuusitisha mkataba huo kati yake na serikali kuu.

Gavana huyo amewalaumu watu kutoka ‘Ikulu’ kwa kutumia mkataba huo wa uhamisho wa majukumu ili  kumhujumu na kumfedhesha

Aliandika katika tweeter mafadhaiko yake akisema  ‘ Acha waniue  au wanipeleke jela wakitaka, ndio waendelee na ujinga zao wakati sitakapokuwa gavana wenu’

Akizungumza na gazeti la The Star,  msaidizi wa kibinafsi wa Sonko Ben Mulwa amesema tayari gavana huyo amewapa mawakili jukumu la kupitia stakabadhi zote husika kabla ya kuwasilisha kesi yake kortini wiki ijayo ili kuukatiza mkataba huo . “ Wiki chache tu baada ya mkataba huo kuanza kutekelezwa tumeshuhudia ukosefu wa heshima kutoka kwa maafisa hao wa Ikulu. Mkataba huo ni wa miaka miwili, hatuwezi kundelea hivi’ alisema.

Sonko  amesema yeye na rais Uhuru Kenyatta ‘walikuwa na nia njema ‘ wakati waliposaini makubaliano hayo  lakini baadhi ya maafisa wake ambao wanamchukia wameuteka mkataba huo ili kumletea soni na ‘kumfadhaisha’

Amesema hadi  sasa hajapewa nakala ya makubaliano hayo ambayo aliyatia saini kabla ya kupata muda wa kusoma yaliyokuwemo.

“ Sikupewa muda wa kutosha kusoma nakala ya makubaliano hayo. Niliambiwa tu  ni mkataba mzuri wa kuleta huduma bora kwa wakaazi wa Nairobi  ninaposhughulikia kesi yangu kortini. Kwa sababu nawapenda nyinyi  watu wa (Nairobi) niliukubali mkataba huo bila hata kuusoma.’ Sonko amesema