Ni Kweli: WHO yasema kuna ushahidi unaoonyesha kuwa corona inaweza kusambazwa kupitia hewa

Shirika la Afya duniani limekiri kwamba kuna ushahidi unaojitokeza kwamba virusi vya corona vinaweza kusambazwa kupitia chembe ndogo ndogo zinazosalia hewani.

''Maambukizi hayo ya kupitia hewa hayawezi kupuuzwa katika maeneo yenye watu wengi, maeneo yaliofungika ama yasio na hewa ya kutosha'', alisema afisa mmoja.

Iwapo ushahidi huo utathibitishwa huenda ukaathiri masharti ya maeneo ya ndani.

Barua ya wazi kutoka kwa zaidi ya wanasayansi 200 ililishtumu shirika la afya duniani WHO kwa kupuuza uwezekano wa maambukizi kupitia hewani.

WHO limesema kwamba kufikia sasa virusi hivyo husambazwa kupitia chembechembe wakati watu wanapokohoa ama kupiga chafya.

Tulitaka kutambua ushahidi, Jose Jimenez, mwanakemia katika chuo kikuu cha Colorado ambaye alitia saini nakala hizo, aliambia chombo cha habari cha Reuters.

''Hili sio shambulio dhidi ya WHO. Ni mjadala wa kisayansi, lakini tukahisi tunahitaji kuelezea umma kwa sababu walikuwa wanakataa kusikiza ushahidi huo baada ya mazungumzo yangu nao'', alisema.

Maafisa wa WHO wametahadharisha kwamba ushahidi huo ni wa mapema na unahitaji kuchunguzwa zaidi.

Benedetta Allegranzi, msimamizi wa masuala ya kiufundi wa WHO kuhusu kuzuia na kudhibiti maambukizi, alisema kwamba ushahidi unaojitokeza kuhusu maambukizi kupitia hewa katika maeneo yalio na watu wengi, yaliofungika, yasioingia hewa safi ambayo yameelezewa, hauwezi kupuuzwa.

Hii leo Shirika la WHO limekiri kwamba kuna ushahidi unaosema kwamba hilo linawezekana katika maeneo fulani kama vile yaliofungika na yale yalio na watu wengi.

Ushahidi huo hata hivyo utalazimika kuchunguzwa zaidi, lakini iwapo utathibitishwa, ushauri wa jinsi ya kuzuia kusambaa kwa virusi hivyo utalazimika kubadilika, na unaweza kusababisha utumizi zaidi wa barakoa mbali na kufuata masharti ya kutokaribiana hususana katika baa, mikawaha na katika usafiri wa umma.