Ni mwisho wa Nasa, Raila Odinga awinda marafiki wapya

Junet, Raila, Mutua, Okoth-compressed
Junet, Raila, Mutua, Okoth-compressed
Muungano mpya unaandaliwa huku chama cha ODM kikitengana na vyama tanzu vya awali vilivyounda NASA.

Kinara wa chama cha ODM anatumia maafikio ya uchaguzi mdogo wa Kibra kusanifisha siasa zake za 2022, huku akitumai kwamba kufaulu kwa BBI kutaleta taswira mpya katika uchaguzi mkuu ujao.

Waziri mkuu wa zamani akiongoza sherehe za kutoa shukran kwa wana Kibra alisema kwamba ushindi huo ni wa taifa nzima.

"Uchaguzi wa Kibra ni mfano kwa taifa nzima kuwa wakenya wana kiu ya mabadiliko," Raila alisema.

Aliongeza kuwa," Imetudhihirishia kuwa wakenya wamechoka na siasa potovu na ufisadi. Pia, imetufafanulia kwamba pesa hazitanunua kura."

Kwa kile kinaonekana kuwa mkondo mpya katika siasa za nchi, kiongozi wa ODM aliwaorodhesha marafiki wapya, baadhi yao wakiwa mahasimu wake wa kitambo.

Kikundi chake kipya kinajumuisha wanachama kutoka Mlima Kenya, Ukambani na maeneo ya Bonde la Ufa.

Mojawapo ya windo kuu la Raila ni naibu wa gavana wa Kiambu James Nyoro ambaye wakati moja alikuwa mshauri katika ofisi ya Ruto kabla ya kuacha kazi hiyo 2015 na kuingia siasa.

Baadhi ya wanachama kutoka timu ya Kieleweke walionaswa kwenye kikosi kipya cha Raila ni mbunge Maina Kamanda, mbunge wa  Cherang’any Joshua Kuttuny na wabunge za zamani Dennis Waweru Dagoretti kusini na Kilemi Mwiria wa Tigania magharibi.

Gavana wa Kirinyaga Ann Waiguru, Spika wa bunge la kaunti ya Nairobi, Beatrice Elachi, mwakilishi wa wanawake wa Wajir Fatuma Gedi miongoni mwa wengine.

Wote hao walishirikiana na chama cha ODM kwa kumpigia debe Imran Okoth huku wakimpuuza McDonald Mariga ambaye alikuwa akigombea kwa chama cha Jubilee.

Mbunge wa Chereng'any Joshua Kutuny anaibuka kuwa mfuasi mkubwa wa Raila katika Bonde la Ufa, eneo linaloaminika kuwa na uungwaji mkubwa wa naibu wa Rais Ruto.

Kutuny alikuwa miongoni mwa walioambatana na Raila Jumapili.

Kutoka eneo la magharibi mwa Kenya, Raila amenasa wabunge wawili kutoka chama cha ANC cha Musalia Mudavadi. Wawili hao ni mbunge mteule Godfrey Osotsi na seneta wa Kakamega Cleophas Malala.

Wawili hao walikuwa wakimuunga mkono mgombeaji wa chama cha ODM Imran Okoth huku wakimpuuza Eliud Owalo wa chama chao cha ANC.

Pia, juhudi za Raila zimemnasa viongozi wa Ukambani ambao ni Kalonzo, pamoja na magavana watatu-  Charity Ngilu, Kivutha Kibwana na Aflred Mutua.