Nigeria yaanza safari ya kuwaondoa raia wake Afrika Kusini

afrika kusini
afrika kusini
Raia wa Nigeria 640 wasajiliwa katika ubalozi wa Nigeria nchini Afrika Kusini na kundi la kwanza la raia hao litaondoshwa Jumatano kufuatia mashambulio dhidi ya raia wa kigeni nchini Afrika Kusini.

Ndege ya Air Peace itaondoka Johannesburg saa tatu kamili asubuhi kwa saa za Afrika Kusini na inatarajiwa kuwasili mjini Lagos kwa saa za Nigeria.

Kulingana na taarifa iliyotolewa na wizara ya mambo ya nchi za nje ya Nigeria kwenye ukurasa wake wa twitter inakadiriwa kuwa idadi ya raia 313 watachukuliwa kutoka Afrika Kusini katika awamu ya kwanza na waliosalia watasafirishwa siku za Alhamisi na Ijumaa wiki hii.

Raia wa Nigeria wanaoishi Afrika Kusini walipewa ofa ya ndege za bure kurejea nyumbani kukwepa vurugu za kibaguzi zinazoendelea Afrika Kusini.

Wizara ya mambo ya Nje ya Nigeri ilisema mmliliki wa Shirika la Ndege la Air Peace yupo tayari kuwasafirisha bure wale wote watakaotaka siku ya Ijumaa.

"Wote watakaotaka huduma hiyo wanashauriwa kuwasiliana na Ubalozi wa Nigeria jijini Pretoria na ofisi ndogo za ubalozi jijini Johannesburg jwa matayarisho muhimu," taarifa ya wizara ilieleza.

Mashambulizi ya biashara zinazomilikiwa na wageni nchini Afrika Kusini zimepokelewa kwa hasira kali na Wanaigeria ambao wanahisi wanalengwa na kuonewa.

Awali waziri wa Mambo ya Nje wa Nigeria Geoffrey Onyeama aliwaambia wanahabari siku ya Jumatano wiki iliyopita kuwa kulingana na taarifa zilizowafikia, hakuna raia wa Nigeria aliyepoteza uhai kwenye ghasia zinazoendelea.

Hata hivyo, alisema watadai fidia kwa biashara zote za raia wa nchi hiyo zilizoshambuliwa.

Nigeria imesusia kuhudhuria Mkutano wa Kimataifa wa Uchumi unaofanyika Afrika Kusini kutokana na ghasia zinazoendelea.

Serikali ya Nigeria tayari iliwaonya raia wake waliopo Afrika Kusini wasisafiri ama kuelekea kwenye maeneo ambayo ghasia hizo zimeshamiri mpaka pale hali itakapotengemaa.

-BBC