'Nilisikia ukemi wa mtoto' mamake msichana aliyebakwa atoa ushahidi

Mahakama moja ya Hola imemhukumu mwanamume mwenye umri wa miaka ishirini kifungo cha maisha kwa kumnajisi mtoto mdogo.

Hakimu Mwandamizi wa Hola Bw. Alloyce Ndege alimpata Doyo Said na hatia ya kumnajisi msichana aliyekuwa na umri wa miaka mitano mnamo Novemba 17, 2017 huko Laza katika mji wa Hola, kaunti ya Tana River.

Mamake msichana huyo (jina lake limebanwa) aliieleza mahakama kuwa Said, ambaye alijulikana vizuri katika familia hiyo kwa jina Akram, alifika nyumbani kwao kutazama habari kwa runinga za saa tatu siku hiyo.

Kwa sababu alikuwa akiitembelea familia hiyo mara kwa mara, haikumjia akilini mamake msichana huyo fikira kuwa Akram angewadhuru wanawe.

Silika ya mama ingemwonya kuwa alikuwa amemkaribisha gaidi wa watoto katika nyumba yake, hasa kwa kuona vile binti yake mdogo alivyomzoea kijana huyo.

Hivyo basi akaamua kutoka nje kumwona jirani yake na kumwacha msichana huyo mdogo pamoja na kakaye, ambaye alikuwa amelala, katika ulinzi wa mshtakiwa huyo.

Hapo ndipo nyang’au huyo alipoyatoa makucha yake aliyokuwa ameyaficha na kuchukua nafasi hiyo kumpeleka malaika huyo chumba kimoja cha malazi na kumnajisi.

Punde si punde, mama mtoto aliingia sebuleni lakini hakuona mtu. Alisikia ukemi wa mtoto katika chumba kimoja, na alipoingia hakuyaamini macho yake.

Akram, ambaye suruali yake ilikuwa ikining’inia magotini, alikuwa amembeba mtoto katika mapaja yake, huku mtoto akilia kwa uchungu.

“Mshtakiwa alishangaa kuniona nimerudi haraka hivyo na akamtupa binti yangu kitandani na kuanza kuvaa nguo haraka haraka,” alisema.

“Nilimkamata kwa nguvu zangu zote huku nikipiga mayowe kuwaita majirani lakini akaniponyoka na kutoroka, huku akiacha kipande cha shati yake na kiatu kimoja.”

Majirani walikuja haraka, lakini mshitakiwa alikuwa tayari ametoweka katika giza la usiku huo, alisema mama huyo.

Alisema alimkimbiza binti yake katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Hola ambako uchunguzi wa kimatibabu ulifanywa na ikabainika kuwa alikuwa amebakwa.

Hapo ndipo walipopiga ripoti katika kituo cha polisi cha Hola, lakini tayari mshatikiwa alikuwa amejipeleka mafichoni.

Ripoti ya daktari iliyotolewa mahakamani ilidhihirisha kuwa msichana huyo alikuwa ameharibiwa sehemu yake nyeti.

Akijitetea, Akram alisema kuwa familia ya msichana huyo ilimsingizia, na kwamba ilikula njama na majirani, afisa wa matibabu na maafisa wa polisi ili kumlimbikizia madai ya uongo.

“Mheshimiwa, familia hii ilikuwa na mipango miovu dhidi yangu, na ndio maana ilikula njama pamoja na majirani, afisa wa matibabu na maafisa wa polisi ili kunilimbikizia madai ya uongo,” alisema.

Alikataa vizibiti vilivyotolewa kortini - kiatu kimoja na kipande cha shati yake – akisema havikuwa vyake.

Lakini hakimu Ndege alishangazwa na vile Akram alivyoenda mafichoni punde tu baada ya tukio hilo na akakamatwa baada ya rafiki mmoja wa jamii hiyo kumuona katika eneo la Mushroom katika mji wa Hola na kuwafahamisha maafisa wa usalama.

Alisema aliridhishwa na ushahidi wa mamake mlalamishi na ile ripoti kutoka kwa daktari na kusema hana shaka lolote kuwa mshitakiwa alitenda kitendo hicho.

Hakimu aliendelea kusema kama mshitakiwa alikuwa hana hatia, hangekuwa amejifanya mwendawazimu wakati alipofikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza na kuisababishia mahakama kupoteza wakati ili yeye mshtakiwa afanyiwe uchunguzi wa kiakili.

“Katika msingi wa ushahidi uliotolewa na vizibiti vilivyoletwa mahakamani, ninakupata na hatia katika shtaka hili na kukuhukumu ipasavyo,” alisema Bw. Ndege.

Alitangaza kuwa mhalifu huyo ni hatari sana na akaamuru apatiwe ushari nasaha na mwelekezo, pamoja na mafundisho kuhusu mapenzi wakati akiwa jela.

Alipewa siku kumi na nne kukata rufaa.