Nimekuwa mgonjwa wa saratani tatu pamoja na Ukimwi - Sally

Ndani ya ilikuwaje hii leo mgeni wetu ni Sally Kwenda ambaye anaishi na virusi vya ugonjwa wa Ukimwi huku pia akiwa mwadhiriwa wa ugonjwa wa saratani mara tatu.

Sally mwenye umri wa miaka 50 anasema kuwa aliugua ugonjwa wa ukimwi mwaka wa 1999.

"Nilienda kupimwa mwaka wa 1999 na nikagundulika kuwa nilikuwa naugua ugonjwa wa Ukimwi. Nilirudi na kumwelezea mume wangu hali yangu ila yeye alikana na kusema kuwa alijua hali yake na hakuwa na ugonjwa huo."

Sally alipogundua hali yake alielewa sababu kuu ya kuwapoteza wanawe wawili huku mmoja akiwa na umri wa miezi miwili. Kutokana na hali hizi zilizomkumba, Sally aliamua kujitoa uhai.

 "Nilimwandikia dadangu mkubwa barua ya kumpa kwaheri kisha nikaelekea zangu Likoni kijitoa uhai. Ferri ilipofika katikati nilijirusha bahari nife. Hatahivyo, mimi sikuzama majini jambo lililonishtua sana na kuwashangaza abiria wa feri hio."

Sally anasema kuwa kabla hajaokolewa alikawia maijini kwa muda unaozidi dakika 10 huku akielea majini licha ya hali kwamba hakuwa anajua kuogelea. Hata hivyo, anasimulia kuwa jambo la ajabu lilitokea kwani alisikia sauti isiyo ya kawaida na kulingana naye yeye anaamini ni mwenyezi mungu aliyemwita.

"Nakupenda sana lakini kwa sasa nenda ukaokoe watu wangu mie ndiye muumba wako."

"Nilipelekwa hospitalini na kisha kutafftiwa daktari. Baadaye nilipelekwa kituo cha polisi na kuulizwa iwapo nina mtu anijuaye. Mume wangu alipoulizwa kama alijua hayo alisema kuwa mie ni mtu mzima na hivyo nilistahili kuwa na maamuzi yangu kivyangu."

Baada ya mambo hayo yote, Sally alipatana na kampuni moja ya ya kibanfsi ya kuwapa watu ushauri iliyomwitia ajira na kumfunza kuwapa ushauri watu wanaoishi na virusi vya ukimwi pamoja na saratani.

Miaka mitano baadaye mumewe aliamua kwenda kupimwa ugonjwa wa Ukimwi na akagunduliwa kuwa amekuwa akiishi na virusi hivyo. Hatahivyo, mumewe Jack alikataa kunywa dawa jambo lililopelekea kifo chake mwaka wa 2012.

 Mwaka wa 2007, Sally aligundulika kuwa na saratani ya mfereji wa uzazi (Cervical Cancer). Saratani hii ilipelekea Sally kufanyiwa upasuaji wa uzazi wake na kisha ukaondolewa.
Pamoja na hayo, Sally amekuwa na saratani ya koloni pamoja na saratani ya Puru. Hata hivyo, Saratani zake zote zilitibiwa kwa kutolewa sehemu husika mwilini. Mwaka 2016, Sally alikuwa amepona magonjwa yote ya Saratani.

Kwa sasa Sally ni mshauri wa wagonjwa wa Ukimwi na saratani huku akiwa mwadhiriwa.

"Ningewaomba watu wote wanaoishi na watu wenye virusi hivi wawape upendo kwani mtu anaweza kuishi na hali hii kwa muda mrefu kwani mimi nimeishi nayo kwa muda wa miaka 20 sasa. Wagonjwa wote watafte dawa pamoja na kuwa na matumaini."