Nina uhakika Ozil na Kolasinac wako tayari kucheza - Unai Emery

kolasinac
kolasinac
Kocha wa Arsenal Unai Emery ana uhakika asilimia mia moja kuwa wachezaji wake Mesut Ozil na Sead Kolasinac wako tayari kurejea katika kikosi chake, baada ya kuwachwa nje ya mechi ya kwanza ya ligi ya EPL dhidi ya Newcastle kutokana na usalama wao.

Wawili hao walikua wamehusika na jaribio la kuibiwa na watu wawili ambao walitiwa mbaroni na kufunguliwa mashtaka. Emery pia anadai wawili hao wako katika hali nzuri ya kimawazo na watafanya vyema.

Mtandao wa kijamii wa Twitter umekubali kujadili ubaguzi wa rangi na kundi moja linalopambana na ubaguzi huo katika soka Kick It Out kwa mara ya kwanza.

Haya yanajiri wakati mshambulizi wa Chelsea Tammy Abraham alipolengwa mitandaoni kwa kukosa mkwaju wa penalty wakati walipopoteza 5-4 kwa Liverpool katika fainali ya Super Cup jumatano usiku. Kick It Out imekuwa ikishinikiza jukwaa za mitandaoni kuchukua hatua dhidi ya ubaguzi huo.

Hayo yakijiri, kocha wa mchezo wa table tennis wa timu ya taifa Fahd Daim anasema kuwa ana imani kikosi chake kitafika katika awamu ya medali katika michuano ya All African games nchini Morocco.

Fahd amekua akifanya mazoezi na timu yake katika ukumbi wa  Kasarani kwa mwezi mmoja kabla ya kuondoka jana kabla ya kuelekea Rabat, Morocco.

Kikosi hicho chenye wachezaji 10 kitaongozwa na Josiah Wandera, Brian Mutua, na  Ken Kojal upande wa wanaume huku Doreen Juma, Nelly Mutuma, na Pamela Glory wakiongoza kikosi cha kinadada.

Timu ya soka ya Kenya ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 15 itaanza kampeni yake katika mchuano wa CECAFA dhidi ya Somalia kesho mjini Asmara, Eritrea. Kenya ambao wako katika kundi A pamoja na wenyeji Eritrea, Sudan na  Burundi watakuwa wanawania ushindi ili kuimarisha nafasi zao za kufuzu kwa awamu ya robo fainali. Kocha msaidizi Elvis Nandwa anadai wako katika hali nzuri na watakua wanatafuta ushindi.

Mabingwa wa zamani wa KPL AFC Leopards waliwalaza Polisi wa utawala mabao 2-0 katika mechi ya kirafiki iliyochezwa jana katika uwanja wa KTTC. Ingwe ilipata mabao yake kupitia Austin Ochieng na Hansel Ochieng, huku wakiziba ngome lao na kuhakikisha wapinzani hawakufunga goli lolote.  Ingwe walimaliza katika nafasi ya 11 na watakua wanawania kushinda ligi msimu huu baada ya zaidi ya miaka 20.