Ningali nalia nikiwa chumbani mwangu nikimkumbuka Laboso, Abonyo asema

ezmnqvgjcropmbqx5d433e60ad31d
ezmnqvgjcropmbqx5d433e60ad31d
Baada ya miezi mitatu tangu kifo cha aliyekuwa gavana wa Bomet Joyce Laboso, Abonyo anasema kwamba bado angali na huzuni, simanzi, na upweke kwa kuondokewa na mke wake aliyempenda sana.

Taarifa ya tanzia kuhusu kifo cha Gavana Joyce Laboso iliwashtua wananchi wengi sana mnamo Julai 29. La kuvunja moyo zaidi ni kwamba Abonyo alijua wazi kwamba maisha ya mkewe yangekatika wakati wowote baada ya kipindi kirefu sana cha matibabu.

"Kumekuwa na ripoti chache sana kutoka madaktari kuhusu visa vya kansa vilivyotibiwa na wagonjwa kupona kabisa baada ya ugonjwa huo kujitokeza tena mwilini kwa mara ya pili," alisema.

"Nimelia sana nikiwa pekee yangu. Kila mara nikifika nyumbani, chumbani mwetu, ninapatwa na hisia na kumbukumbu kuhusu maisha yake hutokea tena upya, ninakumbuka kila kitu na mawazo hayo hunitawala," Abonyo alisema.

Abonyo amesema kwamba yeye hajaamua kupanga upya nyumba yake kwa kuwa yungali na simanzi na uchungu wa kuondokewa na mkewe.

"Wakati fulani niliwaambia madakatari wamwache abakie tu katika hali ya kukosa fahamu kwa kuwa alikuwa akihisi uchungu sana na nafsi yake ya kupona iliendelea kudidimia," Abonyo alisema.

Anasema kwamba ijapokuwa alisaidiwa na marafiki wengi, bado wengine wangali kutimiza ahadi zao.

Aliongeza kusema kuwa hadi sasa hajapanga nyumba yake ikiwemo nguo zao kabatini katika makazi yao ya Sotik na Fort Ternan.

'Hadi sasa bado ninayo picha ya gavana huyo wa zamani, kitabu cha maombolezo na mishumaa minne kwenye kiti kidogo inayoashiria maombolezo nyumbani kwetu Kilimani Nairobi," alisema.

Isitoshe alisema kwamba kila wikendi aendapo kwao Fort Ternan, wao huweka maua mapya kwenye kaburi lake marehemu.

Abonyo alisema kwamba ugonjwa wa kansa ulijitokeza upya hata baada ya Laboso kuonyesha dalili ya kupona awali, na kwa mara ya pili alijua kwamba ugonjwa huo ungemwangamiza.

'Wakati mke wangu alipatikana na ugonjwa huu miaka ya 90 katika Nairobi Hospital, niliacha yote niliokuwa nikifanya na kusafiri hadi nyumbani kwa wazazi wangu Nyalenda Kisumu na kuwalilia kwamba Joyce anaaga dunia," alisema

Ijapokuwa Laboso alinusurika wakati huo, alifichua kwamba wakati Joyce alimpigia simu kwa mara ya pili kwamba alikuwa amepatikana na ugonjwa huo kwa mara ya pili, hakulia jinsi alivyofanya mwanzo.

Abonyo na mwanawe Brian Ochieng' walisema kwamba Joyce  alikuwa katika ziara rasmi Marekani wakati alipoamua kujipima katika MD Anderson Cancer Centre - akiwa na lengo la kupata ufadhili ili kusaidia eneo la Bomet.

"Hapo aliamua kutumia fursa hiyo kujipima. Hakuwa na maumivu yoyote, ila wakati kila mara alikuwa akilalamika kuchoka sana akiwa nyumbani," Abonyo alisema.

Aliendelea kusema kuwa alipopigiwa simu na mkewe kuhusu kupatikana na ugonjwa huo, alimsihi kukatisha safari yake na kurejea nyumbani ili kuanzisha matibabu.

"Nimekuwa mbali kwa miaka 15 na nilidhani kwamba kurejea nyumbani ingenipa fursa ya kujumuika na mama na familia yangu. Kumbe haingekuwa jinsi nilivyotarajia. Imekuwa kipindi cha majonzi," Brian alisema.

Hata baada ya mazishi, Brian anasema kwamba alibakia kwao Fort Ternan kwa majuma mawili baada ya kila mmoja kurudi mijini, kwa kile anasema alihisi upweke.

'Kila mara nikitazama kaburi, moyo wangu huvunjika. Lakini tumejaribu kuyakabili hayo kwa kuwa sisi siyo wa kwanza kufiwa," alisema.