No sex without pay! Mwanamke alivyoanza kumtoza mumewe ‘ada’ ya ngono

sad mama
sad mama
Kwa kweli kuna watu ambao hujichimbia kaburi kisha udongo ukishawafunika wanaanza kutapatapa wakitafuta hewa huku wakipiga ukemi kutaka usaidizi .

Ndio  njia pekee inayoweza kutumiwa kueleza tabia za mwanamke mmoja ambaye alikuwa na mazoea ya kuitisha malipo kutoka kwa mume wake kabla ya kufanya naye tendo la ndoa. Mwanzoni ikaonekana kama mchezo wa wanandoa lakini baadaye ilipozidi na kuwa ada kwamba lazima apewe kitu  au malipo ndipo afanye mapenzi na mumewe, ikawa sasa muda wa kuokoa ndoa yake umepita. Dorcas Mbijiwe* huenda hakujua alichokuwa akifanya ni kibaya au labda kuna ushauri usiofaa ambao alikuwa akipewa na kidudumtu kule nje aliyetaka kumvurugia ndoa. Mume wake Elias anasema  kamwe hajawahi kufanya mapenzi na mke wake kabla hajamlipa ama kumpa ‘ hongo’. Alipowasimulia wenzake masaibu yake, wengi walimcheka lakini idadi kubwa walimhurumia.

Inakuaje mke wako anakutaka umlipe kabla ya kushiriki mapenzi naye?  Wengi walishangaa na hawakupata jibu. Baadaye ikagunduliwa kwamba Dorcas alililelewa na mamake pekee na walipokuwa wasichana waliobaleghe ilikuwa  mazoea tangu utotoni kwamba wangepewa pesa au ahadi ya kitu kabla hawajafanya lolote pale nyumbani.Tabia hiyo maskini aliipeleka hadi katika ndoa yake ila baadaye ilimkosti kwani visanga vyake viliwazidi watu maarifa na ikaamuliwa kweli hatoweza kusaidika.

‘Mke wangu huwezi kumgusa kabla hujaweka pesa mezani. Endapo ungetaka usiku wa starehe naye  lazima uanze kumhonga mapema na asubuhi, anachoitisha umpe’ anasema Elias ambaye huruma katika macho yake inakupa taswira ya mtu  ambaye hakuwa na chaguo lingine ila katumiwa  vibaya kweli .

Kila kilichokuwa kikifanyika ndani ya ndoa yao kilisalia siri hadi wakati Elias alipoanza kujiuliza maswali kuhusu tabia ya mkewe. Maswali yake hayo yalimfikisha kwa rafiki zake ili ajue kutoka kwao endapo nao pia lazima walitakiwa kugharamika kabla ya kushiriki tendo la ndoa na wake zao. Wengi walisema hilo ni jambo geni kwao. Kunao hata waliomwambia Elias kwamba mke wake alikuwa ‘akifanya ukahaba ndani ya ndoa’ kwa sababu anayeuza mwili wake ni kahaba iwe  kwa mumewe au mtu wa nje, wengi walisadiki .

Jaribio la kutaka kujua mbona  Dorcas alikuwa akitaka kulipwa kabla ya  kufanya mapenzi na mume wake halikuzaa majibu yaliyotakiwa. Dorcas alitoa vijisababu   ambavyo vilishtua kuhusu tabia yake. Wanawake wenzake walimtishia kwamba mtindo wake huo ungemfanya mume wake kutafuta ngono nje ya ndoa lakini hakuambilika.

Alipogundua kwamba mkewe hatobadilika, Elias aliamua kuuvunja mwiko na kwa mara ya kwanza, akampa kisomo mkewe kuhusu tabia zake. Hapo na hata akamtaka afungishe virago vyake aondoke akawalipishe watu wengine mwili wake. Dorcas hakujua mumewe katoa wapi ujasiri wa kumwambia hayo lakini maji yalikuwa yamezidi unga na wito wake wa kutaka kusamehewa na Elias haukumtikisa mumewe aliyekuwa tayari keshafanya uamuzi wa kutalakiana naye.