Chineekee! Joyce Akinyi wa Sakata ya Chinedu akamatwa na Cocaine

  Mfanyibiashara mpenda sakata Joyce Akinyi amekamatwa baada ya kupatikana na kilo nne za dawa za kulevya aina ya Cocaine  . Akinyi alikamatwa jumamosi pamoja na washukiwa wengine wawili kwa ulanguzi wa dawa za kulevya . Mfanyibiashara huyo amejipata katika mkondo mbaya wa sheria takriban miaka minne tangu akamatwe na polisi . Katika kisa cha jumamosi ,mfanyibiashara huyo alitiwa nguvuni na polisi katika  eneo lake la burudani la Deep West  ,Langata Road baada ya kunaswa na kilo nne za  podari nyeupe  inayoshukiwa kuwa cocaine. Alizuiliwa katika kituo cha polisi cha Muthaiga pamoja na washukiwa wengine wawili ,mwanamke na mwanamme mmoja raia wa Congo.

 Duru zaarifu kwamba polisi  waliamua kufanya oparesheni katika eneo hilo la burudani baada ya washukiwa kadhaa kukamatwa wakiwa na sachet za  cocaine katika maeneo mbali mbali ya Nairobi . Baadhi ya washukiwa waliokamatwa ndio waliomhusisha Akinyi na  mtandao wa kusambaza dawa hizo za kulevya . Akinyi sio mgeni wa sakata kama hizo kwani mara ya mwisho alipokamatwa mwaka wa 2015  alipatikana na  podari iliyoshukiwa kuwa cocaine .Baadaye aliachiliwa huru pamoja na washukiwa wengine watatu .

Mwaka wa 2013 Akinyi na mbunge Budalangi Raphael Wanjala  walikamatwa na polisi katika barabara kuu ya  Nairobi kwenda Namanga katika eneo la Isinya kwa madai ya ulanguzi wa dawa za kulevya .Baadaye waliachiliwa huru waliposisitiza kwamba walichokuwa wamebeba ni unga wa mahindi ulioagizwa kutoka Tanzania .Wanjala na  Akinyi,  ambao wanadaiwa kuwa wapenzi  pia wamewahi kuzuiliwa nchini India mwaka wa 2008  walipopatikana na shilingi milioni 7.59 ambazo hawakuwa wameeleza maamlaka walikozitoa .Waliachiliwa huru baada ya maamlaka za Kenya kuingilia kati.

Akinyi na mumewe waliyetengana naye   raia wa Nigeria   Anthony Chinedu  wamehusishwa na mtandao wa usafirishaji wa dawa za kulevya na pia wamewahi kugonga vichwa vya habari kwa kuzozania eneo la burudani la Deep West lenye thamani ya mamilioni ya pesa .Baadaye Chinedu alirejeshwa nchini Mwake .