Obama awasili Kenya, atembelea Rais Kenyatta

Aliyekuwa Rais wa Marekani Barrack Obama aliwasili nchini Kenya leo alasiri na kuanza ziara yake ya siku mbili  kwa kumtembelea Rais Uhuru Kenyatta.

Akimkaribisha Rais huyo wa 44 wa Marekani, Rais Kenyatta alimshukuru Bw. Obama kwa kutimiza ahadi yake aliyotoa mwaka 2015 alipozuru Kenya akiwa Rais wa Marekani, kwamba aterejea tena Kenya baada ya kukamilisha kipindi chake cha kuhudumu kama Rais  wa Marekani.

Rais Kenyatta alimpongeza Bw. Obama kwa kuanzisha Wakfu wa Obama ambao unakusudia kuwapa shime vijana kuwa chanzo cha mabadiliko yanayohitajika katika bara hili.

Viongozi hao wawili walikubaliana kwamba vijana barani Afrika wanaweza kuchangia maendeleo kikamilifu endapo uwezo na ubunifu wao utatumika ipasavyo.

Bw. Obama yuko nchini Kenya kuzindua mradi wa Wakfu wa Sauti Kuu unaojumuisha Kituo cha michezo, kituo cha kujiimarisha na kutoa mafunzo ya kiufundi. Mradi huo unasimamiwa na dadake wa kambo Dkt. Auma Obama.

Kwenye kikao ambacho pia kilihudhuriwa na Naibu wa Rais William Ruto na maafisa wengine wakuu serikalini, Rais Kenyatta alimhakikishia Bw. Obama  kwamba viongozi wa Afrika wako tayari kumuunga mkono kuimarisha miradi ya vijana chini ya Wakfu wake.

Katika moyo halisi wa Kenya wa kutunuku wageni zawadi, Rais Kenyatta alimkabidhi Bw. Obama vitabu viwili viitwavyo Aspirations of a generation,youth of Kenya na Kenya at 50. Vitabu hivyo vinasimulia ufanisi  wa vijana na ufanisi uliopatikana katika nyanja mbali mbali nchini kwa kipindi cha miaka 50 iliyopita.

Baada ya kuzindua Wakfu huo wa Sauti Kuu na kuzuru mahala mzazi wake alitoka huko Alego Nyang’oma katika kaunti ya Siaya, Bw. Obama atasafiri kuelekea  Afrika Kusini anakotazamiwa kutoa hotuba ya mwaka wa 16 kuhusu Nelson Mandela jijini Johannesburg.