Katika uamuzi wake hakimu mkuu mkaazi Fredrick Nyakundi alisema mlalamishi hataki tena kuendelea na kesi hiyo na hivyo Sonko hangejibu mashtaka hayo. Mkurugenzi wa mashtaka ya umma alikuwa amewasilisha ombi la kuitaka mahakama kutupilia mbali kesi hiyo baada ya Yakubu kuamua kuachana nayo .
Stakabadhi ya mashtaka ilisema Sonko alimshambulia afisa mmoja mkuu wa polisi mwendo saa sita unusu wakati polisi huyo alipokuwa akitekeleza kazi yake kinyume na ibara ya 103 ya sheria ya huduma kwa polisi ya mwaka wa 2011 . Sonko alishtumiwa kwa kumpiga teke kamanda wa polisi wa eneo la pwani Rashid Yakubu katika uwanja mdogo wa ndege wa Ikanga .
Mashahidi wanne akiwemo Yakubu na maafisa wa polisi James Mwanzia, Michael Muriithi, Fred Sabai, Stephen Mtawa na Ibrahim Ahmed walikuwa wameorodheshwa kutoa ushahidi dhidi ya Sonko.
Kisa hicho kilitokea Disemba tarehe sita wakati gavana huyo alipokuwa akikamatwa katika kizuizi kimoja cha barabarani ili kujibu mashtaka ya ufisadi katika kaunti ya Nairobi. Sonko anakabiliwa na jumla ya mashtaka 19 ya ufisadi, utumiaji mbaya wa maalaka ya afisi yake na malipo yasio halali ya shilingi milioni 357.