Omanga ni miongoni mwa maseneta 6 wanaotaka nafasi ya Kindiki

omanga
omanga
Seneta maalum na ambaye anakabiliwa na utata kwa kutohudhuria mkutano uliokuwa umeitishwa na rais Uhuru Kenyatta, Millicent Omanga ni miongoni mwa maseneta waliowasilisha maombi ya kutaka nafasi ya naibu spika wa seneti.

Soma pia;

Seneta huyo alifika mbele ya kamati ya nidhamu ya Jubilee siku ya Jumatano kueleza sababu za kukosa kuhudhuria mkutano wa kiongozi wa chama.

Alidai kwamba hakupokea mwaliko kuhudhuria mkutano huo.

Maseneta wengine wanaomezea mate kiti hicho ni  Margaret Kamar (Uasin Gishu), Charles Kibiru (Kirinyaga), Isaac Mwaura (Seneta maalum), Judith Pareno (Seneta maalum) na Stewart Madzayo (Kilifi).

Soma pia;

Mchakato wa kutafuta uungwaji mkono kwa wadhifa huo tayari umeanza huku uchaguzi ukiratibiwa kufanyika siku ya Jumanne wiki ijayo.

Spika Kenneth Lusaka siku ya Jumanne alichapisha kubanduliwa kwa Seneta wa Tharaka Nithi Kithure Kindiki katika gazeti rasmi la  serikali na kualika maseneta kuwasilisha maombi ya kutaka wadhifa huo.

Kiranja wa wengi katika seneti Irungu Kang'ata na mwenzake wa upande wa wachache Mutula Kilonzo Junior awali walisema kwamba walikuwa wanafanya mashauriano ili kuwasilisha mgombeaji mmoja ili pasiwepo upinzani baina yao.

Soma pia;

Kulingana na kanuni za bunge, mgombea atatangazwa mshindi kwa wadhifa wa naibu spika ikiwa atapata thuluthi mbili ya kura.

Ikiwa hakuna mgombeaji anayepata 2/3 ya kura, basi duru ya pili ya uchaguzi hufanyika baina ya aliyeshinda na yule aliyemaliza katika nafasi ya pili. Katika duru hii  ya pili yeyote atakayezoa kura nyingi hutangazwa mshindi.