OUT! Barca na Real Madrid wabanduliwa nje ya Copa Del Rey

barca
barca
Barcelona na Real Madrid wamebanduliwa nje ya Copa Del Rey baada ya kupoteza kwa Athletic Bilbao na Real Sociedad mtawalia katika robo fainali. Matumaini ya Barcelona ya kufika fainali ya saba mfululizo ya Copa del Rey yalizimwa walipopoteza 1-0 kwa Bilbao.

Awali Real Madrid iliwashangaza wengi iliponyukwa mabao 4-3 na Sociedad. Hii ina maana kwamba kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2010, fainali ya Copa del Rey haitakuwa Barcelona wala Real.

Msururu wa habari za michezo;

Timu nane zitakua zinawania kunyakua taji la Chapa Dimba Na Safaricom kwa kinda wikendi hii, huku michuano hio ikielekea mkoa wa mashariki.

Washindi wapya watatawazwa baada ya mabingwa watetezi, Super Solico na St. Mary’s Ndovea kuchujwa katika awamu ya kwanza. Upande wa wanaume  Black Panther, shule za  upili za St. Daniel’s na Tumaini pamoja na Biashara FC zitapambana, huku  Ngaaka Talents, Chuo kikuu cha Chuka, Isiolo Queens na Mabuu Queens wakiwania ubingwa upande wa kinadada.

Chelsea na Manchester United wanajiandaa kupambana vikali kuwania saini ya mshambuliaji wa Uingereza na Borussia Dortmund Jadon Sancho. Nyota ya mzaliwa huyo wa Uingereza mwenye umri wa miaka 19, imekua iking'aa katika klabu hio ya Ujerumani na anapigiwa upatu kuzidi kutamba viwanjani.

Hata hivyo, wakala wake wanasema licha ya kuhusishwa na vilabu hivyo watatoa maamuzi mwishoni mwa msimu.

Baada ya kuhusishwa na sakata ya kupanga mechi aliyekuwa kiungo wa kati wa Kakamega Homeboyz  Festo Omukoto amepata pigo lingine, baada ya Western Stima kukatiza mkataba wake jana. Omukoto alikua miongoni mwa wachezaji watatu wa Homeboyz waliopigwa marufuku ya miaka minne ya shughuli zote za soka na Fifa.

Mwenyekiti wa Stima Laban Jobita anasema aliamua kufutilia mbali mkataba wa kiungo huyo, ili kulinda hadhi ya klabu hiyo.

Timu ya raga ya Kenya Sevens itachuana na Afrika Kusini, Ireland na Canada katika kundi B kwenye msururu wa Los Angeles 7s Machi tarehe moja na mbili.

Shujaa watakuwa wanatafuta matokeo mazuri zaidi baada ya kupata alama moja tu katika msururu wa Sydney 7s wikendi iliyopita. Wakati huo huo mabingwa wa Sydney 7s Fiji wako katika kundi A pamoja na Argentina, Ufaransa na Korea. Wenyeji Marekani, Australia, Scotland na Samoa wako katika kundi C huku Uingereza, New Zealand, Wales na Uhispania wakiwa katika  kundi D.

Waziri wa michezo nchini Amina Mohammed amewahakikishia wakenya kwamba nchi hii iko tayari kuandaa  mbio za ubingwa duniani za chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20, mwezi Julai.

Amina anasema serikali imeweka mikakati kabambe ya kuhakikisha michezo hio imekua ya kufana kama ile ya chipukizi wasiozidi miaka18 iliyoandaliwa mwaka wa 2017 Ugani Kasarani. Wajumbe 25 kutoka shirikisho la riadha duniani, wanatarajiwa humu nchini wiki ijayo kufanya ukaguzi wa miundo msingi.

Vilabu vya ligi ya Premier vimepiga kura kubadilisha dirisha la uhamisho la majira ya joto ili kuliainisha na eneo zima la Uropa. Kwa misimu miwili iliyopita, dirisha la uhamisho la Uingereza limekuwa likifungwa siku moja kabla ya ligi hio kuanza. Katika taarifa ligi ya primia inasema makataa yamebadilishwa hadi mwishoni mwa Agosti au mwanzo wa Septemba. Tarehe ya mwaka huu ya kufungwa kwa dirisha hili ni Septemba mosi.

Sofapaka jana ilimteua Mike Mururi kama naibu wa kocha, baada ya kukubaliana mkataba wa miaka miwili. Mururi atakuwa naibu wa John Baraza. Baraza ambaye amekuwa kocha mkuu wa klabu hio awali, alifanya kazi pekee yake baada ya kufutwa kazi kwa raia wa Ureno Divaldo Alves mwezi Novemba kutokana na matokeo duni.

Batoto ba mungu wamefungwa mabao 25 katika mechi 19 na sasa wako katika nafasi ya 9 kwenye jedwali wakiwa na alama  27 points. Muiruri awali alikuwa kocha wa Chemilil Sugar na Kakamega Homeboyz.