‘Pastor alinihadaa nifanye naye mapenzi ili nizae’

woman
woman
Kukosa mtoto ni jambo ambalo wengi huchukulia kwa mzaha lakini  kutana na mwanamke  ambaye hajafanikiwa kupata mtoto ili uweze kujua mahangaiko wanayopitia .

Kwa  Shelly Wacu  kutoka Nakuru, ndoa yake ya miaka saba bila mtoto ilimfanya  kuwa tayari kufanya jambo lolote ili afanikiwe kumzalia mumewe mtoto lakini baadaye  matokeo yake yamekuwa majuto. Baada ya kujaribu njia zote za matibabu na hata miti shamba, shelly hakuweza kupata mtoto na haikuwa rahisi kwake kukubali kwamba yeye ni tasa . Watu wengi sana wakiwemo jamaa na rafiki zake walimtembeza  Shelly kwa watu mbalimbali. Sio waganga, sio waomabaji  na watalaam aina nyingi ili kumsaidia shelly apate mtoto lakini bila mafanikio. Kiasi cha pesa ambacho pia yeye na mumewe  walitumia ili kuweza kupata mtoto kilikuwa cha juu sana na hatimaye mume wake alisalimu amri na kukubali kwamba hangewahi kupata mtoto, lakini kwa Shelly , vita  vyake  vya kuzaa havikuishia hapo .

Aliendelea kutafuta msaada kwa kila aliyemwambia kwamba kuna mtu anayeweza kumsaidia apate mtoto na ikawa rahisi sana kumshawishi kufanya chochote .Hapo ndipo ngoma ilipoanza wakati mhuburi mmoja wa kanisa jipya mjini Nakuru alipokuja na kupata sifa za kuweza kusuluhisha mambo mengi ikiwemo mtu kukosa mtoto .Wafuasi  wake mjini Nakuru walimuita kuwa  nabii na wanawake kwa wanaume waliokuwa na msururu wa matatizo mbalimbali walipiga foleni katika kanisa lake kupata msaada . Hapo ndipo Shelly alipoamua pia kucheza kamari ajaribu kupata usaidizi wa mhubiri huyo ili apate mtoto .

Alipokutana na  mhubiri huyo, hakuna kilichomfanya ashuku kwamba alikuwa mlaghai na  akamuombea na kumtaka awe na imani kwamba siku moja atapata mtoto .  Kisha akampa ratiba ya kuja kwa maombi kila jumapili na hata siku ambazo watu hawakuwa kanisani ili aombewe . Kimoja baada ya kingine, siku moja mhubiri akamwambia kwamba lazima ashiriki naye mapenzi ndiposa ndoto yake ya kupata mtoto itimie . Washirika wengine wa kanisa hilo walijitokeza na kumuambia Shelly kwamba afanye kila anachoambiwa na nabii  na  angeweza kupata mtoto . Kuna waumini wa kanisa hilo waliojitokeza katika ushuhuda kanisani wakidai kwamba hakuwa na watoto lakini baada ya usaidizi wa nabii waliweza kufanikiwa kupata watoto .Hilo lilimpa sana matumaini Shelly kwamba siku moja angepata mtoto .

Baada ya kutafakari pendekezo hilo la mhuburi huyo kutaka kulala naye ili aweze kupata mtoto, Shelly alihofia kumwambia mume wake kuhusu  hatua hiyo akiogopa kwamba angekataa. Kwa hivyo, alipiga moyo konde na kulala na mhubiri akiwa na matumaini  kwamba atapata mtoto .Ole wake! Kilichofanyika baadaye sio tu cha kuhuzinisha bali ni jambo la kuvunja moyo kwani ufichuzi ulitolewa kwamba mhubiri huyo alikuwa  keshafanya hivyo kwa wanawake kadhaa  mbeleni na kwamba utabiri wake ni ulaghai ! Shelly alijua kweli amejiingiza katika shimo ambalo  hangweza kujitoa .  Muda sio mrefu uvumi ulianza kuzagaa jinsi ambavyo yeye na mhubiri huyo walilala pamoja na  hata walikuwa wapenzi . Kabla hajajua cha kufanya mume wake alikuwa tayari keshaarifiwa kuhusu alichofanya na huo ndio uliokuwa mwisho wa ndoa yake . Mhubiri alianza kutafutwa na polisi kwa makosa mengi ya ulaghai baada ya watu kadhaa kujitokeza na lalama mbalimbali .Baadaye Shelly alilazimika kurejea kwao akiwa na mzigo wa aibu za kulala na mhubiri , fedheha ya kuachwa na mumewe na  kuonekana kama mjinga aliyehadaiwa  ili kulala na mhubiri feki .