PATANISHO: Mke wangu anataka nijenge nyumba kwanza ili arudi

Reuben aliomba apatanishwe na mkewe bi Sophia akisema kuwa wawili hao walikosana mwaka jana.

Reuben alijieleza,

"Nilishikwa hapo Muthaiga kwani mimi ni dereva wa bodaboda ambaye alikuwa amebeba abiria wawili na nikafungwa Industrial area. Mke wangu alikopa fedha na kuja kunitoa ndani kisha mchungaji wangu alifurushwa kanisani na mke wangu alikuwa miongoni mwa wale walienda naye.

Nilipomkanya kuzungumza naye hakuskia na kwa hasira nikamzaba kofi na hapo akakasirika na kuondoka."

Wawili hao wamekuwa kwa ndoa ya miaka mitano na pamoja wana watoto watatu ambao mkewe aliondoka nao.

Aliongeza akisema mkewe alimwambia aende ajenge nyumba kisha atafute wazee ambao watazungumza nao.

Alidai kuwa anamshuku yule pastor kwa sababu yeye ndiye humpigia mkewe simu wala sio yeye na isitoshe walipozazana, mkewe alihakikisha amefungwa jela kwa siku nne kabla ya kuchukua kila kitu nyumbani na kuondoka.

Juhudi za watangazaji wetu kumfikia Sophia haikufua dafu kwani alikuwa amezima simu.

Alipopewa fursa ya kuzungumza na mkewe alimuomba mkewe msamaha na kuomba arudi ili waishi kama zamani.