(Picha) Ibada ya wafu ya marehemu gavana Joyce Laboso

Mamia ya waombolezaji siku ya Alhamisi waliungana katika kanisa la All Saints Cathedral mjini Nairobi kwa ibada ya wafu ya marehemu Gavana wa Bomet Joyce Laboso.

Waombolezaji miongoni mwao jamaa wa familia yake, marafiki, mawaziri, wanasiasa na wafanyibiashara walianza kuwasili mwendo wa saa mbili asubuhi.

Naibu Rais William Ruto na Gavana wa Nairobi Mike Sonko waliwasili mwendo wa saa nne na dakika 25.

Skrini kubwa pia zilitundikwa nje ya kanisa hilo ili kuwapa nafasi waliokuwa wamekosa nafasi ndani ya kanisa pia kufuatilia ibada.

Ibada iliongoza na Askofu Ernest Ng’eno akisaidiwa na Canon Sammy Wainaina.

Mumewe Laboso, Edwin Abonyo alivalia suti ya samawati na kiraba cha rangi ya zambarau

Mwana wa kiume wa kwanza wa Laboso alisoma wasifu wa marehemu mamake.

Wanawake wawili magavana waliosalia Charity Ngilu wa Kitui na Anne Waiguru waliongoza katika kusoma somo la ibada.

Laboso ambaye kufikia kifo chake alikuwa gavana wa Bomet alifarika Jumatatu wiki hii.

Alifariki akipokea matibabu katika Nairobi Hospital baada ya kuugua saratani kwa muda mrefu.

Alikuwa amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahtuti juma moja tu baada ya kuwasili nchini kutoka India alikokuwa akipokea matibabu.

Laboso ambaye alitajwa na waombolezaji kama mwanamke shupavu, alikuwa mwanamke wa kwanza kuwa gavana wa Bomet baada ya kumlambisha sakafu aliyekuwa gavana Isaac Rutto katika uchaguzi wa mwaka 2017.

Aliwakabili wapinzani wake waliojaribu kutumia ndoa yake na Edwin Abonyo kutoka eneo lingine kusambaratisha azimio lake kuwa gavana.

Naibu wake Hillary Barchok amekuwa akiendesha shughuli za kaunti tangu aondoke nchini kwenda kupokea matibabu na anatarajiwa kuapishwa kama gavana mpya baada ya mazishi.