Pigo kwa United huku Maguire akitarajiwa kuwa nje kwa mda

Beki wa Manchester United Harry Maguire ataendelea kukaa nje kwa muda bila kushiriki mechi yoyote.

Hii ni kutokana na jereha la mfupa wa nyonga analouguza. Kufikia sasa michuano ambayo hatashiriki haijulikani. Lakini wasiwasi wa United ni kwamba hawakutarajia angekaa nje kwa muda mrefu baada ya kupewa moyo na Ole Gunnar Solskjaer, aliyesema kuwa jeraha hilo lilikuwa dogo. Maguire aliumia Manchester United ilipokuwa ikicheza na Wolves jumamosi iliyopita.

Borussia Dortmund haipo tayari kumwachilia nyota wake Jadon Sancho kununuliwa mwezi huu na baadhi ya vlabu vinavyommezea mate hususan vile vya Uropa.

Borussia inahofia kwamba hawana mchezaji atakayechukua nafasi yake endapo atagura ikiongeza kuwa kandarasi yake klabuni humo itakamilika mwishoni mwa mwaka 2022.

Miongoni mwa klabu zilizoonyesha nia ya kumnunua Sancho mwenye umri wa miaka 19 ni pamoja na Chelsea, Manchester City, Manchester United, PSG Real Madrid na Barcelona.

Tusker ilipanda kileleni mwa ligi ya KPL baada ya kuilaza Kisumu All stars 2-0, huku Kakamega Homeboyz wakiwapiga Zoo Kericho 1-0 na kupanda hadi nafasi ya pili.

Ulinzi stars nao waliwanyuka Wazito FC 1-0 , huku KCB ikitoka nyuma na kuibwaga Sofapaka 2-1 nao Kariobangi Sharks waliwafunga Bandari 1-0. Western Stima waliwaadhibu Mathare United 2-1.

Chemilil sugar nao walisalia kushikilia mkia licha ya kupata ushindi wao wa kwanza msimu huu wa 1-0  dhidi ya Nzoia Sugar. Katika mechi ya mwisho hapo jana goli la dakika la mwisho la Sammy Odero, liliisaidia Posta Rangers kuilaza AFC Leopards 2-1.

Kocha mkuu wa timu ya Posta Rangers Sammy Pamzo Omollo anadai licha ya kuwalaza AFC Leopards 2-1 katika mechi ya ligi jana timu zote mbili zilicheza vizuri na yeyote angeshinda mechi hio.

Pamzo pia amewapongeza Ingwe kwa mchezo wao na anawapigia upato kufanya vyema msimu huu.

Mshambulizi Leroy Sane, anakaribia kurejea kwenye mazoezi ya Manchester City baada ya kuwa nje kwa miezi mitano akiuguza majeraha.

Mzaliwa huyo wa Ujerumani mwenye umri wa miaka 23 alikua nguzo katika timu hio na kocha mkuu Pep Guardiola anasema kurejea kwake kutawapiga jeki wanapoelekea wakati mgumu wa msimu.