Polisi wawekwa katika hali tahadhari huku DPP akigonga ngome ya Ruto

SECURITY
SECURITY
NA LUKE AWICH

Idara ya polisi jana usiku ilikuwa katika hali ya tahadhari katika maeneo kadhaa ya Rift Valley baada ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma Noordin Haji kuagiza kukamatwa kwa watu 28 akiwemo waziri wa fedha Henry Rotich.

Tahadhari hiyo ilitolewa punde tu baada ya Haji kutangaza kukamatwa kwa Rotich, katibu wa kudumu Kamau Thugge na mwenzake wa Jumuia ya Afrika Mashariki Susan Jemutai kwa tuhuma za ukiukaji wa sheria kuhusiana na ujenzi wa mabwawa ya Arror na Kimwarer.  Watu wengi 25 walikamatwa katika eneo la Rift Valley hatua iliyozua hofu kuhusu hali ya usalama. Wengi wa washukiwa wanatoka eneo la Bonde la Ufa na walifanya kazi katika Halmashauri ya ustawi wa Kerio Valley.

Habari zaidi:

"Shirika la ujasusi nchini –NSIS linashauri kuimarishwa kwa usalama katika eneo hilo ikizingatiwa historia ya eneo hilo. Kwa hivyo tumetuma maafisa wa kutosha kushika doria kutuliza hali yoyote ikiwa machafuko yatazuka.," Alisema afisa wa cheo cha juu katika eneo la Rift Valley.

Mwaka 2007, zaidi ya watu 1,300 waliuawa baada ya machafuko kuzuka katika eneo hilo kutokana na utata uliyotokana na uchaguzi mkuu wa urais.  Siku ya Jumatatu DPP alitowa onyo kali kwa yeyote ambaye huenda alikuwa anapanga kuzua ghasia.

Habari zaidi:

"Twafahamu kwamba ufisadi hujibu na kwamba huenda kuna baadhi ya watu wanaopanga kutumia matukio ya hivi punde kuzua vurugu, tumeweka mikakati kutathmini njama kama hizo, na tutazikabili vilivyo,” alisema.

Vita dhidi ya ufisadi vimegonga sana ngome ya Naibu Rais William Ruto baada ya sakata ya mabwawa kuhusisha wandani wake, miezi kadhaa baada ya kupuuzilia mbali madai ya kuwepo kwa sakata hiyo “uongo mtupu”

Haji alimweka Rotich katikati ya sakata hiyo iliyolenga kufyonza mabilioni kutoka kwa mradi huo wa ujenzi wa mabwawa wa kima cha shilingi bilioni 63.

Ni wazi kwamba upande wa naibu rais William Ruto haujafurahishwa na matukio hayo, kiongozi wa wengi katika seneti Kipchumba Murkomen alipuuzilia mbali kukamatwa kwa washukiwa na akitaja hatua hiyo kama “publicity stunt being used to play politics.”

IMETAFSIRIWA NA DAVIS OJIAMBO