Polygamy sio Mchezo: Unachohitaji kujua kuhusu kuwa na mke zaidi ya mmoja

polygamy
polygamy
Polygamy. Ni jina la kiingereza ambalo hazua mhemko miongoni mwa akina dada na bashaha katika  nyoyo za wanaume . Lakini kando na  mafunzo ya kidini ,itikadi za kijamii na  kanuni za maadili na ustaarabu ,ndoa za mke zaidi ya mmoja ni  jambo ambalo limezua mgawanyiko wa maoni na kupandisha hisia   kwa wengi .Katika chapisho hili  ambalo [pia linategemea mafunzo na   mwongozo wa kidini  ,tujaribu kuchanganua na kukueleza unachofaa kufahamu kuhusu  ndoa za polygamy .  Bro ,kabla ya kuamua kupata mke wa pili hakikisha kwamba unayafahamu haya na pia unaweza kujibu baadhi ya maswali yanayojipenyeza katika mjadala huu.Pia ,kuna vidokezo kwa wanawake wanaojipata katika ndoa hizi ,kwa kutaka wenyewe au kwa kujipata katika hali kama hizi .

 Mbona?kwa nini mke wa pili ?

Dhana potovu ambayo huwaingiza wengi katika shimo la kujichimbia ni kuoa mke wa  pili ,ili kurekebisha makosa katika ndoa yako na mke wa kwanza . Sababu zinazofanya ndoa yako na mke wa kwanza kuvurugika  huenda zikaibuka tena na kuchafua  ndoa yako na mke wa pili ,kwa hivyo ni vyema sana mtu kujiuliza iwapo  sababu zake za kutaka mke wa pili ,zinamridhisha  na pia kukubalika  na wengi .

Pia kama mwanamme unafaa kuwa tayari  kuvuna ,ulikotoa jasho .Huwezi kutaka manufaa yote  ya ndoa za mke zaidi ya mmoja  ilhali hutaki kuwajibika .

So ,kabla ya kuamua kumleta mke wa pili ,jiulize-Mbona namhitaji mke wa pili?

 

2.Kuwatengea muda wako kwa usawa.

Baada ya  kuvuka swali la kwanza la mbona unamhitaji mke wa pili ,fahamu kwamba  iwapo sababu zako zitakuridhisha ,unafaa kujihami na ufahamu na ujuzi wa jinsi ya kuhakikisha kwamba unawaridhisha wote kwa njia ilio sawa ili kupunguza  uhasama  na migogoro . Malumbano katika ndoa hizo ni jambo ambalo haliwezi kuepukika lakini ili kupunguza visa hivyo ,hakikisha kwamba unajigawanya  njia ilio sawa  katika muda unaotumia kwa kila mmoja wao . Endapo patatokea ishara kwamba unatumia muda mwingi  kuwa na mmoja wao ,basi itaonekana kana kwamba umempenda zaidi . Unapopata muda na mumeo ,kama mke katika ndoa kama hii ,usijipe uzito wa fikra kwa kumwingiza mawazoni mke  mwenza . Unapobaki pekee yako wakati mumeo yupo kwa mke wa pili ,tumia muda huo kama wako wa kibinafsi.Jishughulishe na unachopenda unapongoja zamu yako kuwa na muda bora na mumeo .Kama mwanamme katika ndoa hii,usiingize  masuala yako na mke mwingine katika uhusiano  wako na Yule ambaye umepata muda naye .

3.Uhasama wa uke-wenza

 Hili halitowahi kukoma .Mwanamke anaweza kukuambia kwamba hana tatizo na wewe kuwa na mke mwingine ,lakini moyoni na katika fikra anasumbuliwa  na  hatua hiyo . Kama mwanamke katika ndoa  ya wake wengi ,hakikisha kwamba  unatilia maanani uhusiano wako na mumeo pekee .Usije ukatia fikrani kwamba kuna mtu wa tatu katika ndoa yenu .Unapopata muda naye ,muda huo ni wenu nyinyi wawili wala sio muda wa ndoa ya watu watatu . Usimchukulie mke mwenza kama mpinzani wako  , badala yake jishughulishe na  jitihada za kuboresha uhusiano kati yako na mumeo . Kwa kawaida wakati mke mmoja anapohisi hapendwi au hahitajiki katika ndoa ,yeye humtwika lawama mke mwenza  hatua ambayo huwa kiini cha  uhasama mkali sana ambao unaweza kudumu kizazi baada ya kingine .Angazia kuhusu mazuri anayokufanyia mumeo  na pia ufahamu kwamba mke mwingine naye pia ana shauku zake na huenda pia anafikiri unapendwa zaidi yake .

  1. Kukabiliana na wivu

 Hakuna makali mazito kama wivu wa kimapenzi na hasa kutoka kwa mwanamke .Wivu ni kitu ambacho kinaweza kuzima mapenzi yoyote kati yako na mumeo . Njia bora ya kuepuka hilo ni kuangazia kile ulicho nacho .Ilimradi una vitu ambavyo ni muhimu kwako ,sio lazima uwe na kila ambacho mke mwenza amepewa . Ni jukumu la mumeo kuhakikisha kwamba mahitaji yenu kama wanawake katika ndoa ya pamoja yanashughulikiwa, kwa hivyo anafaa kukupa kila unachohitaji . Usichukulie kila jambo kama mashindano ya kufika ,Chukulia kila kitu kama fursa ya kujiimarisha kivyako na mumeo .  Ingawaje ni vugumu kabisa kumaliza wivu katika ndoa za mke zaidi ya mmoja ,uzingativu wa hayo unaweza kupunguza  tatizo hilo

  1. Kutafuta na ugavi wa raslimali(Pesa)

Pesa au mali huwa sababu kuu ya mizozo katika ndoa za wake wengi . Kama mwanamme katika ndoa kama hizo hakikisha kwamba kila mke wako ana njia ya kujipa kipato na pia kuna mfumo wa jinsi pesa zako zinavyogawanywa kati ya familia zako kwa njia sawa . Mara nyingi kinachozua  purukushani ni madai kwamba familia ya mke mmoja imependelewa kwa kupewa mgao mkubwa  wa raslimali za familia . Ni bora kuhakikisha kwamba iwapo una mali inayozaa manufaa kama vile  kodi kutoka kwa nyumba za kupanga, inagawanywa mapema ili kila mke ajue kwamba hiki na hiki ni chake na kingine na kile na cha mke mwenza .Hatua hiyo itakuepushia  mizozo ya mara kwa mara kuhusu mmoja kudai kwamba mwenzake amechukua mgao mkubwa .Pia usije ukajjiingiza katika ndoa za wake wengi iwapo huna mali au  raslimali kuwatunza wanawake hao.

6.Watoto

Ni bora endapo watoto katika ndoa hizi watafahamu kuanzia mwanzo kwamba wapo katika familia moja .Aghalabu uhasama kati ya wake wenza huwafanya watoto  kukomaa na uhasama dhidi ya wenzao wa nyumba nyingine .Iwapo hujajitumbukiza katika ndoa kama hii ,anza kufikiria kuhusi jinsi maisha yatakavyokuwa kati ya watoto wako kutoka kwa bibi zako wawili .

  1. Kusuluhisha Mizozo

 Babu zetu walikuwa katika ndoa za wake wengi kwani waafrika tangu jadi  ni watu wa familia hizi ila tofauti ni  kwamba katika enzi hizo ,wazee walikuwa na busara katika kusuluhisha mizozo kati ya bibi zao ili kuepuka kuonekana kana kwamba wamempendelea mmoja wao .Wanaume wa siku hizi wameshtumiwa kwa kuwa wazembe  na hutafuta njia za mkato wakati wa kushughulikia mizozo baina ya wake zao kwa kuegemea  upande mmoja ili kuzima malumbano zaidi .Unapopendelea upande mmoja ,unapanda mbegu ya usahama ambayo huota na kushika mizizi kwa muda mrefu sana . Katika kusuluhisha mizozo hakikisha unazisikiza pande zote kwanza  kabla ya kufanya uamuzi .

 

  1. Wazi wazi au kisiri ?

Hili ndio swali ambalo huwakumba wanaume wengi kuhusu kupata mke wa pili .Unajiuliza iwapo unafaa kumwoa mke wa pili kisiri au wazi wazi ,ulimwengu mzima ujue kwamba ni mkeo . Mambo ya siri yana  adhabu .Umewahi kuyasikia hayo ya wazee waliooa wake wengi kisiri kisha wakajulikana tu siku ya maazishi  ya mzee.Mzigo huo ni mbaya na mzito sana kwa jamii yako .Ni bora  iwapo unaamua kupata mke wa pili kuweka mambo wazi kuanzia mwanzo.Hata iwapo umejipata pabaya  kwa kumtunga mimba  msichana wa mtu kisha mkakubaliana kuoana ,usimfiche mkeo .Tafuta mbinu na muda bora wa kuzungumza naye .

  1. Jamaa na Familia .

Ni vyema jamaa zako uwaeleze kuhusu  hatua yako  ya kuwa na mke wa pili .Hili huzuia uvumi na  propaganda  kuenezwa baina za wake zako kwani kila jamaa anaibuka na maneno ya  kumweleza mke wa kwanza au wa pili .Hili huzua machungu kati ya wahusika katika ndoa kama hizi .Baadaye utapata familia yako imegawanyika kwa sababu kuna dada zako wasiozungumza na mke wako wa pili nao kaka zako kamwe hawamtaki mkeo wa kwanza .Hakikisha kwamba msimamo wako unafahamika na wote na wanaheshimu kauli zako .

  1. Umoja ni Nguvu .

Endapo   wake zako watakubali kuwa marafiki basi  sawa …una bahati .Iwapo wataamua kwamba kila mtu aishi kivyake ,maskini kazi yako itakuwa nzito  .Lakini kama mwanamme ,hakikisha  kwamba unajaribu kadri ya uwezo wako kuwafanya wafahamu kwamba ushirikiano kati yao ni jambo muhimu sio tu kwa ndoa yenu bali  pia kufanikisha maazimio ya familia yenu kubwa .

Iwapo utapata ujasiri wa kuoa mke wa pili au umeridhika na Ndoa yako ya mke mmoja ,ni vyema kufahamu kila hatari na manufaa ya unakojiingiza .