Radio Africa yaongoza kwa wingi wa kusikizwa nchini Kenya

Kampuni ya Radio Africa imeimarisha makali yake kwa kutajwa kuwa na stesheni ambazo zina wafuasi na wasikilizaji wengi humu nchini Kenya. Kulingana na matokeo yaliyotolewa na shirika la kitaifa, Classic fm, Radio jambo, na Kiss fm ambayo yanamilikiwa na Radio africa ni baadhi za radio ambazo zinasikizwa sana.

Classic fm inaongoza katika orodha hiyo ikiwa na wasikilizaji millioni 1.5 huku kipindi cha “Maina and Kingangi” kikiwakabaa wengi koo.

Radio Jambo inachukua nafasi ya pili likiwa na wasikilizaji millioni 1.18 huku kipindi cha patanisho inayofanikishwa na watangazaji Gidi na Ghost kikiwateka wengi sikio.

Kiss fm ilijikatia tikiti ya nambari tatu ikiwa na wasikilizaji millioni 1.12 huku wasikilizaji watapata kusikia sauti geni kuanzia wiki ijayo Andrew kibe akiwa usukani akisaidiwa na Kamene Goro.

Kulingana na matokeo hayo, Radio africa kwa sasa ina asilimia 48 ya usikilizaji huku wakiwa na malengo ya kuongeza idadi ya wasikilizaji wake, hii ni baada ya Gukena fm, Smooth fm, East fm, na Homeboyz radio kujiunga na kampuni hiyo.