Raila asema atatangaza mipango ya 2022 baada ya mchakato wa BBI

Raila
Raila
Kiongozi wa ODM Raila Odinga amesema atatangaza mipango yake ya uchaguzi wa 2022 baada ya kutamatika kwa mchakato wa BBI . Odinga amesema anazingatia hatua kadhaa lakini uamuzi wake utakuwa wazi baada ya kukamilishwa kabisa kwa  utaratibu mzima wa BBI.Odinga amesema kwa sasa yeye na rais Uhuru Kenyatta wataangazia mwafaka wao wa handshake na  atasalia kimya kuhusu siasa za urithi wa 2022.

Raila  ameongeza kwamba makubalaino yake na Uhuru kusitisha uhasama yalilenga kudumisha Amani nyakati za uchaguzi .

“  Rais hatazoungumzia uchaguzi wa 2022,mimi pia Sitazungumzia uchaguzi huo . Nitazungumza kuhusu 2022 baada ya kutamatika kwa mchakato wa BBI, Raila amesema katika mahojiano na Runinga ya Citizen jumanne usiku .

Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa bwana Odinga kuzungumza kuhusu anavyopanga kushughulikia uchaguzi wa 2022 ingawaje kuna ishara kutoka kwa washirika wake kwamba huenda analenga kugombea kiti cha urais kwa mara ya tano .

Naibu mwenyekiti wa chama cha Jubilee David Murathe na  katibu mkuu wa muungano wa vyama vya wafanyikazi Cotu ,Francis Atwoli  wamedokezea kwamba Raila  ndiye atakayemrithi rais Kenyatta .

Lakini katika mahojiano hayo ,Raila alisema wanaotoa pendekezo hilo wana haki yao ya kidemokrasia kutoa maoni yao.