Rais akutana na magavana huku ufanisi wa Ajenda 4 kuu ya maendeleo ukipewa kipau mbele

Rais Uhuru Kenyatta leo aliandaa  Mkutano Mkuu wa nane  wa Ushirikishi wa Serikali ya Kitaifa na zile za Kaunti ambapo ufanisi wa utekelezaji wa mipango ya  Nguzo Nne za Ajenda Kuu ya Maendeleo  ulijadiliwa.

Rais aliongoza mkutano huo katika Ikulu ya Nairobi ambao pia ulihudhuriwa na Naibu wa Rais na Mawaziri ambapo viongozi walizungumzia kuhusu kujitayarisha kukabiliana na majanga, ufisadi na kulipa madeni yaliyosalia.

Rais ambaye alielezea kuridhika kwake na  hatua zinazoendelea za kutekeleza mipango ya nguzo nne za ajenda kuu ya maendeleo inayohusiana na utoaji wa huduma za afya kwa wote, ujenzi wa nyumba za ghamara nafuu, utengenezaji bidhaa na kujitosheleza kwa chakula, alizishukuru serikali za kaunti kwa kufungamana na serikali ya kitaifa katika kutimiza harakati hizo.

Serikali ya kitaifa na zile za kaunti zinashirikiana kutekeleza Nguzo Nne za Ajenda Kuu ya Maendeleo kupitia ‘Mfumo wa Utekelezaji Mpango wa Nguzo Nne za Ajenda Kuu ya Maendeleo kati yao’.

Kuhusu matayarisho ya kukabiliana na majanga, Kiongozi wa Taifa alizisifu serikali za kaunti kwa kuongoza harakati za kukabiliana na mafuriko na maporomoko ya ardhi yaliyokumba nchi hii mwaka jana.

Alisema  kwamba Mfumo wa Kukabiliana na Hatari na Utaratibu wa Kutoa Misaada unaotayarishwa utasaidia kulainisha jinsi ya kushughulikia majanga nchini.

"Bila shaka harakati hizi hazitapunguza tu dhiki kwa watu wetu siku za usoni wakati wa mafuriko na majanga mengine, bali pia utasaidia kuokoa raslimali kwa mipango na miradi mingine ya kijamii,” kasema Rais.

Rais Kenyatta alisema kwamba Kenya imepiga hatua kubwa tangu kuanzishwa kwa mfumo wa serikali za ugatuzi ambao ulianza kutekelezwa wakati wa kipindi cha kwanza cha Serikali ya Jubilee.

Alisema licha ya ufanisi mkubwa ulioafikiwa, kuna changamoto ambazo zastahili kukabiliwa ndiposa mfumo huo uweze kutimiza lengo lake kikamilifu.

Rais alitoa mfano wa madeni yaliosalia na ufisadi kuwa baadhi ya changamoto zinazowazuia Wakenya kufurahia manufaa ya ugatuzi kikamilifu.

Aliyataja madeni yaliosalia kuwa hujuma kwa wafanyibiashara ambao alisema wanapokea hasara.

“Bado kuna madeni yaliosalia katika afisi za uhasibu ingawa bidhaa na huduma husika ziliwasilishwa zaidi ya mwaka mmoja uliopita.

"Naamini sharti sote tujitolee kulipa madeni hayo yote kwa sababu kwa kutotimiza wajibu wetu tunahujumu sio tu utendakazi wa uchumi lakini pia tunawaumiza watu wetu waliokopa pesa ili kutoa huduma,” kasema Rais.

Kando na sehemu hizo nne za maudhui, kikao hicho kilijadili ripoti kadha za Kamati ya Kiufundi ya Uhusiano kati ya serikali ya kitaifa na serikali za Kaunti na pia ripoti za Baraza la Bajeti na Uchumi.

Vile vile walijadili ripoti ya Tume ya Mishahara na Marupurupu kuhusu usimamizi wa gharama ya mishara ya wafanyikazi wa umma ambayo imeongezeka mno.

Kikao hicho hufanyika kila mwaka na kilibuniwa kuwa jukwaa la kushauriana kuhusu masuala ya serikali ya kitaifa na zile za kaunti.

Magavana hao waliongozwa katika mkutano huo uliofanyika Ikulu na Gavana Wycliffe Oparanya wa Kaunti ya Kakamega ambaye ndiye Mwenyekiti wa Baraza la Magavana.