Rais ataka wazazi kukoma kulazimisha watoto kuzingatia mitihani na digrii pekee

uhuru kenyatta
uhuru kenyatta
Rais Uhuru Kenyatta hapo jana aliwaambia wazazi kuacha kuwashinikiza watoto wao kujipatia shahada za digrii na kuzingatia mitihani tu na badala yake kusisitiza kukuza talanta zao chini ya mtaala mpya was elimu unaosisitiza vipawa na ustadi.

Alisema mtaala huo mpya unawapa watoto wa Kenya tumaini na wanafunzi fursa ya kuimarisha vipawa na uwezo wao.

“Tunashinikiza na kukaza watoto kupita mitihani na kujipatia shahada za digrii kutoka vyuo vikuu. Watoto wetu hawana nafasi ya kukua kama watoto,” kasema Rais Kenyatta.

Kiongozi wa Taifa alizungumza katika Jumba la Mikutano la Kenyatta alipoongoza ufunguzi rasmi wa Kongamano la Tatu la Kitaifa kuhusu Mageuzi ya Mtaala wa Elimu.

Alisema kila mototo ana kipawa  na jukumu la wazazi ni kukuza talanta hiyo.

“Natufanye kazi pamoja kukuza ujuzi na kustawisha vipawa vya watoto wetu,” Rais aliwaambia wazazi huku akiwaonya dhidi ya kuwalazimisha watoto kusomea taaluma  fulani kama vile udaktari "hata pale mtoto anaogopa kuona damu”.

Alisema wazazi mara nyingi hukosa kutambua uwezo wa wanafunzi hata kama watoto wao wangeweza kuwa wanamziki na wasanii mashuhuri.

“Tunafaa kutayarisha watoto wetu kuwa magwiji wa teknolojia ya mawasiliano kama Bill Gates na Steve Jobs wa siku zijazo,” kasema Rais akitoa mfano wa Wamarekani hao wawili waanzilishi wa makampuni makubwa ya teknolojia ya Microsoft na Apple mtawalia.

Kiongozi wa Taifa alidokeza kwamba utekelezaji kamili wa mtaala huo mpya utachochea mabadiliko makubwa katika mfumo wa elimu na kulinda maslahi ya wanafunzi wote licha ya uwezo wao.

“Wanafunzi wote wakiwemo wenye mahitaji maalum watapewa fursa ya kuimarika katika nyanja zao za uwezo na maslahi,” Kasema Rais akiongeza kwamba mabadiliko ya mtaala yamejikita katika mchakato unaotegemea thamani.

Alisema Kenya haina lingine ila kujiwianisha na ukuaji wa haraka kote ulimwenguni na mabadiliko makubwa ya teknolojia kwa kuhakikisha wafanyikazi wake wanapata maarifa ya kisasa humu nchini na kimataifa.

“Mabadiliko hayo ni muhimu iwapo tunataka kuwa na elimu bora ambayo inawafanikisha wanafunzi kushindana vizuri kwenye sekta ya wafanyikazi ulimwenguni,” kasema Rais.

Akigusia mafanikio ya utekelezaji wa mtaala, Rais alisema Serikali iko tayari kutekeleza awamu ya Gredi 4 mwaka ujao na akapongeza tume ya kuwaajiri walimu nchini (TSC) kwa kuwafunza walimu 113,223 kutoka shule za umma na za kibinafsi kuhusu mtaala huo mpya.

Alitoa changamoto kwa Wizara ya Elimu na Tume ya Kuwaajiri Waalimu nchini TSC kudumisha kasi hiyo akisema "waalimu wanastahili kuwa mashujaa wetu wakuu kubadilisha mtaala wetu”.

Kabla ya kongamano la leo, Wizara ya Elimu iliandaa mashauriano kuhusu ubora wa elimu katika Kaunti zote 47 mbali na kuandaa makongamano 11 ya sekta mbali mbali mbeleni ambayo yalitoa nafasi kadhaa kwa washika dau kutoa kauli zao kuhusu mtaala mpya wa elimu.

Msomi maarufu wa Ghana na Naibu Waziri wa Elimu ya Msingi na Sekondari Dkt. Yaw. O Adutwum alikuwa mzungumzaji mkuu kwenye kongamano hilo ambalo vile vile lilohutubiwa na Waziri wa Elimu Prof. George Magoha na Afisa Mkuu wa tume ya TSC Nancy Macharia miongoni mwa wengine.