Rais awatakia Waislamu wote Eid Mubarak

Rais Uhuru Kenyatta ametuma ujumbe wa kheri njema kwa waislamu wote nchini, wanaposherehekea siku kuu ya Eid hapo kesho.

Rais anasema tunapoadhimisha siku hio, tusiwasahau maskini katika jamii. Rais ambaye yuko nchini Canada anasema serikali inafanya kila iwezalo ili kila mkenya aweze kufikia mahitaji ya kimsingi.

Soma ujumbe wake mfupi

Wakenya wenzangu,

Tunapojiunga na ndugu na dada zetu Waislamu kusherehekea Eid-Ul-Fitr na mwisho wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan, natutenge muda kutafakari juu ya kanuni za utu, ukarimu, huruma na kujitolea kuambatana na musimu huu.

Natushukuru kwa sababu ya baraka nyingi ambazo nchi yetu ya Kenya inaendelea kunehemeshwa, kwa ajili ya amani na usalama dhidi ya maadui wetu wa ndani na kigeni, kwa ajili ya ustawi katika kilimo chetu, biashara na ahadi ya siku zijazo zenye matumaini.

Tunapoadhimisha sherehe hizi, tusisahau wale wasiobahatika miongoni mwetu kwa wakati huu. Wenye mahitaji ya chakula, makaazi, ajira na huduma za afya.  

Serikali yangu, kupitia ajenda Kuu Nne za Maendeleo, inajibidiisha kuhakikisha taifa ambalo kila raia ana uwezo wa kukimu mahitaji yake ya kimsingi ikiwemo lishe bora kwa kuhakikisha kuwepo kwa chakula, kunufaika na huduma bora za afya, makaazi ya gharama nafuu na ajira kupitia ustawi wa viwanda.  

Ili kutimiza haya, sharti tushirikiane kwa umoja, amani na upendo kama watoto wazalendo wa taifa hili tukufu. 

Kwa hivyo nawashauri hii leo kuzingatia moyo Mubarak wa sherehe hizi na kuwahusisha wengine kwenye baraka zenu. 

Kwa ndugu na dada zetu Waislamu, Nawatakia Eid Mubarak. 

Asante.