Rais Kenyatta aamrisha Wizara husika kulinda ubunifu wa vijana wa Kenya

Rais Uhuru Kenyatta ameamrisha wizara ya Elimu na ile ya Ustawi wa Viwanda kuanzisha mchakato wa kunakili na kulinda maoni ya kisayansi, miradi na ubunifu wa vijana wa Kenya.

Wizara hizo vile vile zitashirikiana na mashirika mbalimbali kubuni mkakati wa kuwasaidia wanasayansi wachanga kulinda hati zao miliki na mikataba ya kisheria na waekezaji.

Akizungumza baada ya kufungua rasmi maonyesho ya pili ya wanasayansi wachanga katika Jumba la KICC kwa lengo la kuwapa vijana uwezo, Kiongozi wa Taifa alisema Serikali yake inapania kuanzisha mfumo kama ule unaotumiwa nchini Ireland kuwasaidia vijana.

Wengine waliozungumza kwenye hafla hiyo walikuwa Waziri wa Elimu Prof. George Magoha, Katibu katika Wizara ya mafunzo tekelezi Dkt. Kevit Desai pamoja na Balozi wa Ireland humu nchini Fionnuala Quinlan.