Rais Kenyatta aomboleza kifo cha aliyekuwa Katibu wa Bunge la Taifa Justin Bundi

justin bundi
justin bundi
Rais Uhuru Kenyatta ametuma risala ya rambi-rambi na faraja kwa familia, marafiki na jamaa wa aliyekuwa Katibu wa Bunge la Taifa Justin Bundi ambaye alifariki mwishoni mwa wiki kutokana na saratani.

Akimtaja kuwa mtumishi wa umma aliyekuwa na ufahamu mkubwa wa taratibu za bunge na aliyejitolea mno, Rais alisema marehemu Bundi pia alijidhihirisha kuwa afisa mwenye uwazi na wa kutegemewa.

“Kujitolea kwa marehemu Bundi katika kazi yake kulimfanya apande ngazi za madaraka kutoka Mkuu wa Tarafa katika uliokuwa utawala wa mikoa hadi kuwa Katibu wa Bunge la Taifa, ambapo tena alitoa uweledi na ufahamu mkubwa wa michakato ya bunge, yote yakilenga kuimarisha maisha ya Wakenya wenzake,” kasema Rais.

“Ushauri wake na kufanya kazi na wabunge ambao ni wakilishi wa raia ulimwezesha kufahamu na kutambua changamoto zinazotukabili kama taifa na hivyo kuhakikisha kanuni zote za kikatiba kuhusu miswada inayowasilishwa katika Bunge la Taifa zinatimiza matarajio ya Wakenya,” kaongezea Rais.

Rais alisema marehemu Bundi ameacha alama ya kudumu sio tu nchini Kenya bali katika kanda nzima hasa baada ya kufanya kazi kama Katibu wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki.