Rais Kenyatta apokea risala ya kheri njema kutoka kwa Baba Mtakatifu

baba mtakatifu
baba mtakatifu
Rais Uhuru Kenyatta amepokea risala ya kheri njema na baraka kutoka kwa Baba Mtakatifu Francis.

Baba Mtakatifu alituma risala hiyo alipopita anga ya Kenya akiwa safarini kurejea mjini Roma baada ya kukamilisha ziara yake kwa mataifa matatu ya Msumbiji, Madagascar na Mauritius.

Katika risala yake ilyotumwa kwa njia ya redio na kunukuliwa na wadhibiti wa Safari za Ndege wa Kenya, Baba Mtakatifu ambaye ni kiongozi wa kanisa Katoliki ulimwenguni alitangaza baraka za amani na kheri njema kwa taifa la Kenya.

"Rais Uhuru Kenyatta, natoa salamu zangu za kheri njema kwako na watu wa Kenya baada ya ziara yangu ya utume katika nchi za Msumbiji, Madagascar na Mauritius."

"Nawaombea baraka za amani na maisha mema," kasema Baba Mtakatifu Francis.

Baba Mtakatifu aliwasili jijini Maputo, nchini Msumbiji tarehe 4 Novemba kwa ziara ya siku tano katika mataifa ya kusini mwa Jangwa la Sahara ambapo alizuru Madagascar kwa siku mbili na kukamilishia ziara yake nchini Mauritius.

Baba Mtakatifu Francis alizuru Kenya mwezi wa Novemba mwaka wa 2015 katika ziara yake ya kwanza barani Afrika na kuwa Baba Mtakatifu wa pili kuzuru Kenya baada ya Baba Mtakatifu John Paul II aliyezuru Kenya mara tatu.