Rais Kenyatta ataka Bunge kukomesha mzozo wa mgawo wa fedha kwa kaunti

Rais Uhuru Kenyatta leo ametoa wito kwa Bunge la Kitaifa na Seneti kukomesha mzozo kuhusu Mswada wa Mgawo wa Mapato wa mwaka huu ili kuwezesha kuatolewa kwa fedha kwa serikali za kaunti.

Alisema Wabunge wanastahili kuchukua hatua mara moja kuhakikisha kaunti zinapata mgawo wao wa fedha  kwa sababu kucheleweshwa zaidi kutawanyima Wakenya huduma wanazohitaji.

Hata hivyo Rais aliwakumbusha Wabunge kwamba serikali haina fedha za kutosha hivyo basi wanahitaji kufahamu kwamba fedha zile Serikali ya Kitaifa imekuwa ikigawia kaunti ni nyingi kupita kiwango kilichowekwa katika katiba.

“Katiba inasema tugawie kaunti kiasi kisichopungua aslimia 15. Katika kipindi cha mwaka mmoja, niliongeza kiwango hicho hadi aslimia 30,” kasema Rais huku akitoa wito wa kuzingatiwa ukweli katika shinikizo la kutaka fedha zaidi kugawiwa serikali za kaunti.

“Kwa nini msipitishe mswada huo ili watu wapate huduma na kuafikia makubaliano ili tutoe fedha kwa serikali za kaunti?” kaendelea kusema Rais.

Rais alisema nchi hii haina raslimali za kutosha na viongozi hawafai kukaa na kutenda mambo kana kama fedha zimezajaa kote na Kenya ina “rasli mali zisizo na kipimo”.

Kiongozi wa Taifa alisema viongozi pia wanafaa kubadili mawazo na ufahamu wao kuhusu ugatuzi kwa sababu mfumo huo wa utawala haumanishi mashindano kati ya ngazi hizo mbili za serikali.

“Hii ni mifumo miwili ya serikali inayosaidiana kutoa huduma kwa wananchi,” kasema Rais.

Alisema mfumo wa serikali ya ugatuzi unahudumia Wakenya na kile kinachohitajika ni viongozi kubadilisha mbinu zao za uongozi.

“Natambua  kwamba ugatuzi unafanya kazi. Kile tunachohitaji sasa ni kuzingatia ajenda ya kutoa huduma kwa raia waliotuchagua,” kasema Rais.

Kiongozi wa Taifa alizungumza hayo baada ya kufungua rasmi jengo la Ugatuzi Plaza ambamo mna Bunge la Kaunti ya Nakuru.

Alisema viongozi waliochaguliwa wanadaiwa na wapiga kura na njia ya pekee ya kuwalipa ni kuwahudumia kikamilifu.

Rais alisema alifurahishwa na ukarabati na upanuzi wa jengo hilo la Ugatuzi Plaza huku akipongeza Waakilishi katika Bunge la Kaunti ya Nakuru kwa kuweka maslahi ya wananchi mbele ya yale  ya kibinafsi kufuatia uamuzi wao wa kutoenda safari za nchi za kigeni.

Wakati huo huo, Rais Kenyatta alitoa wito kwa viongozi kupunguza siasa na kuangazia huduma kwa wananchi.

Alisema amani na umoja ni nguzo muhimu za maendeleo ya nchi kwa sababu waekezaji wataweka fedha zao mahali penye usalama.

“Nisaidieni kuunganisha wakenya pamoja.Nawakikishia kwangu mna mshirika wa maendeleo,” kasema Rais aliyehutubia Waakilishi wa Bunge la Kaunti ya Nakuru wakati wa kikao katika bunge hilo.

Kikao hicho pia kilihutubiwa na Gavana wa Nakuru Lee Kinyanjui, Seneta Susan Kihika na aliyekuwa Mbunge wa Nakuru Mjini Magharibi Samuel Arama na wengineo.

-PSCU