Rais Kenyatta atia saini Miswada sita kuwa sheria ukiwemo Mswada wa kuimarisha Huduma ya Vijana kwa Taifa

Rais Uhuru Kenyatta leo katika Ikulu ya Mombasa alitia saini Miswada Sita kuwa sheria ukiwemo Mswada wa  mwaka huu wa 2018 wa kuimarisha Huduma ya Vijana kwa Taifa.

Sheria ya Huduma ya Vijana kwa Taifa ya Mwaka 2018 inabadilisha Sheria ya Huduma ya Vijana kwa Taifa kifungu nambari 208 kwa kuanzisha Huduma ya Taifa ya Vijana kama Shirika ambalo wajibu wake utahusisha kuanzisha na kuendesha  shughuli  za kibiashara.

Hatua hiyo inakusudiwa kuhakikisha Huduma ya Vijana kwa Taifa inajitegemea kwa kushughulika na biashara za kujikimu kifedha kuiwezesha kuendesha shughuli zake.

Miongoni mwa mabadiliko mengine, sheria ya Huduma ya Vijana kwa Taifa ya Mwaka wa 2018, inabuni Baraza la Huduma ya Vijana kwa Taifa ambalo litasimamiwa na Mwenyekiti atakayeteuliwa na Rais na ambalo litakuwa na jukumu la kuunda sera, uangalizi, na usimamizi wa kawaida wa Huduma hiyo.

Miswada mingine iliyotiwa saini kuwa sheria ni Mswada wa Masoroveya wa Ujenzi wa mwaka wa 2017, Mswada wa Marekebisho wa Sheria za Bunge wa Mwaka wa 2018, Mswada wa mwaka huu wa  Marekebisho ya Sheria za Vyama vya Akiba na Mikopo na Mswada wa mwaka huu wa Marekebisho ya sheria za Masoko ya mtaji.

Vile-vile, Rais Kenyatta alitia saini kuwa Sheria Mswada wa mwaka huu wa Marekebisho wa nakala za karatasi za ngozi  za  Mgao wa Mapato ya Serikali za Kaunti uliopitishwa na Bunge la Seneti na lile la Taifa.  Sheria hiyo mpya inarekebisha Sheria ya Ukusanya Ushuru ili kuondoa mpangilio wa tatu kujumuisha misaada ya kifedha inayotolea kwa masharti na washirika wa kimaendeleo masuala ambayo hayakuwa yamejumuishwa katika kifungu hicho cha sheria, kama ilivyokuwa imeidhinishwa hapo mbeleni.

Miswada hiyo iliwasilishwa kwa Rais na Spika wa Bunge la Taifa Justin Muturi na Mwenzake wa Seneti Kenneth Lusaka. Wengine waliokuwepo ni Mkuu wa Sheria Paul Kihara,  Katibu wa Bunge la Taifa Michael Sialai na Katibu wa Bunge la Seneti Jeremiah Nyegenye.