Rais Kenyatta atia saini mswada wa marekebisho ya thamani ya ardhi

Rais Uhuru Kenyatta ametia saini miswada miwili kuwa sheria kwa lengo la kuimarisha kujitosheleza kwa chakula na matumizi bora ya ardhi nchini.

Rais ambaye hapo mbeleni alikuwa ametia saini Mswada wa Unyunyizaji Maji Mashamba kuwa sheria, leo katika ikulu ya Nairobi, alitia saini Mswaada wa Marekebisho ya Thamani ya Ardhi. Miswada yote ni ya mwaka huu wa 2019.

Sheria ya unyunyizaji maji mashamba inatafuta kulainisha ustawi, usimamizi na udhibiti wa shughuli za unyunyizaji maji mashamba, huku sheria ya thamani ya ardhi ikitafuta kuleta usawa wa kubashiri uhakika wa viwango vya thamani ya vipande vya ardhi, kodi ya nyumba, ushuru unaotozwa kugharamia shughuli za ubadilishanaji mali na kulipa ridhaa pasipo kuleta hali ya kutoeleweka kwa shughuli hizo.

Sheria ya Unyunyizaji Maji Mashamba inakusudiwa kuunga mkono uthibiti wa uzalishaji wa chakula kwa kubuni Halmashauri ya Kitaifa ya Ustawi wa Unyunyizaji Maji Mashamba na kufafanua majukumu ya Serikali ya Kitaifa na za kaunti katika kushirikisha shughuli za unyunyizaji maji mashamba nchini.

Halmashauri hiyo ambayo itabuniwa chini ya sheria mpya imepewa jukumu la kustawisha na kuimarisha muundo msingi wa unyunyizaji maji mashamba kwa maeneo ya ardhi ya serikali ya kitaifa na ya umma mbali na kutoa msaada wa huduma za unyunyizaji maji mashamba kwa miradi ya wenye mashamba ya kadri na yale madogo-madogo kwa ushirikiano na serikali za kaunti.

Sheria hiyo mpya pia inazipatia kaunti mamlaka ya kuanzisha vitengo vya kunyunyizia  maji mashamba ili kutimiza mahitaji ya kaunti binafsi.

Mbali na kulainisha kodi ya kukadiria thamani ya mashamba, kodi ya nyumba, ushuru unaotozwa kugharamia shughuli mbalimbali za kuhamisha mali na mchakato wa kulipa ridhaa, sheria ya marekebisho ya thamani ya ardhi pia inanuiwa kurahisisha kupata ardhi kwa utekelezaji wa miradi ya umma ya muundomsingi.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali Kennedy Ogeto ambaye aliandamana na Spika wa Bunge la Taifa Justin Muturi na mwenzake wa Seneti Ken Lusaka, Kiongozi wa wengi katika Bunge la Taifa Aden Duale na Kiongozi wa wengi kwenye Seneti Kipchumba Murkomen aliwasilisha miswada hiyo kwa Rais kuitia saini.

-PSCU