Rais Kenyatta awaambia viongozi waige mfano wa marehemu Laboso

uhuru joyce laboso
uhuru joyce laboso
Rais Uhuru Kenyatta hapo jana aliwaataka viongizi kuiga mfano wa marehemu Gavana wa Bomet  Dkt. Joyce Laboso ambaye alisema alikuwa kiongozi mtumishi mwema.

Rais alisema marehemu Laboso alitumikia familia yake, waliomchagua na Wakenya wote kwa unyenyekevu na kujitolea na kufaulu kutimiza mengi katika maisha ambayo yanaonekana machoni pa Wakenya wote.

Â

“Alikuwa mkarimu na alijitolea kuwasaidia watu wa Sotik, Bomet na Wakenya kwa jumla. Hakufanya hayo yote kwa majivuno bali kwa uangalifu na yote aliyofanya ni wazi kwetu sote,” kasema Rais.

Alisema hata ingawa alifaulu kufanya mengi akiwa mbunge, Naibu wa Spika na hata akiwa Gavana, marehemu aliishi maisha ya unyenyekevu na kamwe hakujivuna bali aliishi vyema na watu wote.

Rais ambaye alisema haya katika ibada ya mazishi ya marehemu Gavana wa Bomet huko Fort Ternan, Kaunti ya Kisumu alimuomboleza Dkt. Laboso kama kiongozi ambaye alidhihirisha hadhi kuu huku akiongeza kwamba kamwe hakutumia vibaya nyadhifa za uongozi kujifaidi kibinafsi.

“Mlikuwa na uwezo kufanya kazi za kila aina na kutumia nafasi yenu ya kuwa karibu na serikali ya kitaifa na ya kaunti. Hamkufanya hivyo. Hivyo basi mlituonyesha maana ya kuwa kiongozi mwadilifu," Rais Kenyatta alipongeza familia ya Gavana Laboso.

Rais alimpongeza mumewe marehemu Dkt. Edwin Abonyo kwa kujenga familia yenye ufanisi licha ya tamaduni duni, mila na imani zilizowatatiza wakitafuta ufanisi. Â

Kwenye mazishi hayo yaliyoandaliwa katika Shule ya Upili ya Kandege na kuhudhuriwa na Naibu Rais Dkt. William Ruto na kiongozi wa upinzani Raila Odinga, Rais alisema familia ya Dkt. Abonyo na marehemu Gavana Laboso ni mfano unaostahili kuigwa na Wakenya wote.

“Vile vile umetuambia jinsi ulivyopambana na kushinda ukabila na maswala yote mabaya ambayo yalisemwa lakini Dkt. Laboso hakuyazingatia moyoni. Aliyapuuzilia mbali yote na kuangazia yenye manufaa na kile ambacho angewafanyia wengine na wala sio matusi,” kasema Rais.

Alisema iwapo Wakenya wote wataiga mfano wa marehemu Gavana na familia yake, nchi hii itabadilika na kudumisha amani na umoja na kupokea heshima isiyo kifani bara ni Afrika na kote ulimwenguni.

Kuhusu maendeleo, Rais alitoa chanagamoto kwa mbunge wa eneo hilo James Onyango K'Oyoo kushirikiana na Gavana wa Kisumu Profesa Anyang Nyong'o kutambua miradi anayoweza kutekeleza kupitia serikali ya kitaifa akisema anataka kukumbukwa na wakaazi wa Muhoroni kwa maendeleo na sio tu kwa kuhudhuria mazishi.

Naibu wa Rais Ruto alisema anaunga mkono kikamilifu juhudi za Rais za kuunganisha Wakenya kupitia kwa mkakati wa Building Bridges akiongeza kwamba nyakati za siasa chafu, chuki na ukabila ziliisha kitambo.

Naibu wa Rais alimpongeza Rais kwa hatua  zinazochukuliwa na serikali kukabiliana na saratani hapa nchini.

Aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga aliwataka wakenya kuchagua wanawake zaidi katika nyadhifa za uongozi akisema wachache ambao wamepewa majukumu kama hayo kama vile marehemu Laboso wamefanya vyema.

Wengine waliozungumza katika mazishi hayo yaliyohudhuriwa na maelfu ya waombolezaji kutoka kote nchini ni pamoja na waliokuwa Makamu wa Rais Kalonzo Musyoka na Musalia Mudavadi, Gavana wa Kisumu Profesa Anyang Nyong’o na Mwenyekiti wa Baraza la Magavana aliye pia Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya.