Rais mstaafu Moi bado amelazwa hospitalini, siku 20 baadae

Rais mstaafu Daniel Arap Moi bado amelazwa katika hospitali ya Nairobi siku 20 baada ya kurudishwa hospitalini.

Moi alilazwa tena hospitalini siku mbili tu baada ya kuruhusiwa kwenda nyumbani.

Mkuu wake wa mawasiliano, Lee Njiru wakti huo alisema kuwa rais huyo wa zamani alikuwa anafanyiwa tu uchunguzi wa kawaida wa kiafya.

Kutoka wakati huo, Moi amekuwa katika kitengo cha watu mashuhuri hospitalini hio ili kuwezesha uchunguzi wa kila siku na matibabu muhimu.

Siku ya jumatatu kupitia mahojiano kwa njia ya simu, Njiiru aliambia gazeti la The Star kuwa Moi amekuwa akishughulikiwa na timu ya madaktari wanaoongozwa na daktari David Silverstein.

Alisema kwa sasa Moi amepona lakini madaktari wanahisi anapaswa kupata nguvu kwanza kabla ya kuruhusiwa kwenda nyumbani.

Alisema kuachiliwa kwake kutoka hospitalini kutategemea na ushauri wa daktari.

"Mzee bado yuko hospitalini lakini anaendelea vizuri. Tutatoa taarifa kuhusu hali yake Jumatano. Kwa sasa, tunafuata tu ushauri wa madaktari," alisema.

Njiru alisema taarifa hiyo, hata hivyo, itatolewa tu ikiwa ni lazima.

"Hakuna kitu cha kushangaza juu ya afya ya Mzee. Tunajua ni mtu wa kimataifa anayependwa na watu wengi na lazima wawe na wasiwasi juu ya ustawi wake. Naweza kuthibitisha kwamba hakuna kitu cha kupea watu wasiwasi." alisema.

Njiru, hata hivyo, alisema uvumi mwingi unaozunguka kwenye mitandao ya kijamii kuwa mzee amekufa unaletea familia madhara zaidi.