Rais Mstaafu Mwai Kibaki aadhimisha miaka 88 ya kuzaliwa

Rais Mstaafu Mwai Kibaki anaadhimisha miaka 88 ya kuzaliwa kwake hii leo.

Kibaki ambaye alikuwa rais wa tatu katika taifa hili anakumbukwa sana kwa uongozi wake ulioinua uchumi wa taifa kwa kiasi kikubwa.

Alichukua hatamu za uongozi kutoka Rais Daniel Moi ambaye alitawala taifa hili kwa miaka 24.

Alipotawazwa mnamo Disemba 2002, wakenya walihisi mabadiliko mengi kutokana na utendakazi wake. Ijapokuwa miaka mitano ya mwisho katika uongozi wake kulishuhudiwa ghasia na fujo baada ya uchaguzi mkuu, wanafalafa wengi wanasema kwamba alifanya mengi mazuri ya kukumbukwa.

Haya ni baadhi ya maendeleo aliyoyatekeleza:

Ruwaza ya 2030

Mwai Kibaki alibuni Ruwaza ya 2030 akiwa na nia ya kuimarisha wananchi.

Ruwaza hiyo ilikuwa imebuniwa na nguzo kuu ambazo zilikuwa ni uchumi, miundo msingi, elimu na siasa.

Elimu

Alianzisha elimu bila malipo katika shule za msingi. Katika mpango huo, idadi kubwa sana wanafunzi ilishuhudiwa shuleni.

Lakini baadaye mafawidhi walijiondoa katika mpango huo wakilalamikia ubadhirifu wa fedha.

Aidha Kibaki aliidhinisha na kuongeza idadi ya vyuo vikuu nchini.

Barabara na mawasiliano

Katika kipindi cha miaka 10, takriban kilomita 7,000 za barabara zikiwemo za viungani zilijengwa. Kujengwa kwa barabara hizi ziliongeza ajira kwa wakenya kwa kiasi kikubwa.

Aidha, barabara kuu ya Thika ilijengwa katika kipindi hicho kwa kima cha shilingi bilioni 31.

Afya

Anakumbukwa kwa kukabiliana na maradhi ya Ukimwi na Malaria. Katika uongozi wake wagonjwa walipata dawa za kuzuia makali ya ugonjwa huo bila malipo.

Pia, alitwika jukumu wizara ya afya jukumu la kusambaza vyandarua vya kuzuia mbu hususan kwa wanawake wajawazito.

Wachanganuzi wa siasa wanasema kwamba kipindi cha uongozi ulikuwa wa manufaa kubwa huku mkopo wa deni kutoka mataifa ya nje ukidhibitiwa kinyume na vile wanavyosema wanavyosema wakosoaji wa serikali ya sasa kwamba Rais Uhuru anakopa fedha kiholela.

Aidha, Kibaki anakumbukwa kwa ucheshi wake katika hotuba zake, huku maneno kama"Pumbavu, Bure kabisa" yakitoka kinywami mwake kila mara anapoonyesha dalili za kuudhika.

Naibu wa Rais William Ruto amemtumia salamu za heri njema katika siku hii, huku akitaja maendeleo yake katika taifa, uongozi wake dhabiti na ucheshi uliotawala katika hotuba zake nyingi.

Anapoadhimisha siku hii, Wakenya wamepongeza kutokana na maendeleo yake alipokuwa rais wa tatu wa taifa hili.

Miongoni mwa waliomtakia kila la kheri ni Naibu wa Rais William Ruto kwenye mtandao wake wa Twitter.