Rais Uhuru Kenyatta afunguka kuhusu deni na Ruto,nafasi ya waziri mkuu

Rais Uhuru Kenyatta ameonyesha kwa mara ya kwanza nia ya kutomuunga mkono Ruto katika uchaguzi ujao wa 2022.

Akihutubia viongozi wa eneo la mlima Kenya siku ya Ijumaa, Uhuru alieleza kuwa hajawahi kutoa tamko la atakayemrithi.

Rais alikuwa ameandaa kikao na viongozi kutoka eneo hilo kujadili ubaridi wa kisiasa pamoja na nyufa katika chama tawala cha Jubilee.

Mkutano huo ulikuwa na viongozi takriban 3,000.

Rais pia alisema yaliyo moyoni kuhusu nafasi ya waziri mkuu nchini,

“Sina ufahamu wowote wa mapendekezo ya BBI ila nasikia baadhi ya watu wakisema kuwa Uhuru Kenyatta anataka kuwa waziri mkuu. Siwezi kujali iwapo nitapata cheo kama hicho ila sasa tutatue maswala tuliyo nayo kwanza..."

Katika ziara hiyo,Rais alipigia debe BBI na kuwaomba waunge mkono mapendekezo yatakayotolewa.

Rais aliweka wazi kuwa urafiki wake wa Handshake na Raila Odinga haumaanishi anamuunga mkono kisiasa.

Alisema Handshake inahusu mipango ya kuleta amani miongoni mwa jamii zote hapa nchini.

Aidha, Uhuru alionekana kujawa na ghadhabu kuhusu viongozi wa eneo hilo ambao tayari washaanza siasa za urithi.

”Najua na nawashukuru kwa kuwa mnafahamu hamkunichagua mimi pekee. Hata hivyo, sijakuwa nikisikia kutoka kwa baadhi yenu hapa mkizungumzia mambo muhimu. Kila mara nasikia tu kuhusu 2022 na matusi. Nashangaa ni lini tutawasaidia wananchi? Wakati wa kupiga kura utafika tena. Sijawahi kusema nitamwachia nani kiti,” Uhuru alifoka.

Ruto hapo awali amenukuliwa kusema kuwa hana deni la kisiasa na mtu yeyote.

Kwa sasa, jopo la kamati lililokuwa linakusanya mapendekezo ya BBI lishamaliza na linasema kuwa lipo tayari kumkabidhi rais ripoti hiyo.