Rais Uhuru Kenyatta amemuomboleza Jaji mstaafu Daniel Aganyanya

Daniel Aganyanya
Daniel Aganyanya

Rais Uhuru Kenyatta amemuomboleza Jaji mstaafu Daniel Aganyanya akisema alikuwa mzalendo mashuhuri aliyethamini utawala wa sheria.

Katika risala yake kwa jamaa, ndugu na marafiki wa Jaji Aganyanya, aliyefariki akiwa na umri wa miaka 82 baada ya kuugua mshtuko wa moyo, Rais alisema jaji huyo wa zamani alikuwa shupavu katika vita dhidi ya ufisadi aliyepinga uovu huo hadharani.

“Jaji mstaafu Aganyanya ni mwanasheria aliyethamini uhuru wa mawazo. Alitetea bila uoga utawala wa sheria na aliamini uhuru wa kujisimamia kwa asasi za serikali hasa uhuru wa mahakama,” kasema Rais.

Huku akiongeza kwamba: “Justice Aganyanya atakumbukwa kama mwanasheria mwadilifu ambaye alisimamia alichoamini ni chema kwa nchi yake. Na akiwa Jaji, alikuwa mtu wa kuheshimika na kielelezo chema ambaye aliacha mfano bora katika sekta ya sheria.”

Rais Kenyatta alisema amehuzunishwa mno na kifo cha Jaji Aganyanya na akamuomba Mwenyezi Mungu kuifariji familia yake wakati huu mgumu wa maombolezo.

“Naomba Mwenyezi Mungu awafariji na kuwapa nguvu  wakati huu wa majonzi. Nawaombea,” kasema Rais.

Marehemu Aganyanya alistaafu kutoka Idara ya Mahakama ambako alihudumu katika Mahakama ya Rufaa mnamo mwaka wa 2012 baada ya kutimiza miaka ya kustaafu ya  umri wa miaka 74.