Rais wa Brazil Bolsonaro apatikana na virusi vya corona

Brazil
Brazil
Rais wa Brazil Jair Bolsonaro amegundulika kuwa na virusi vya corona.

Kiongozi huyo amekuwa akipuuzilia mbali janga la Covid-19 akiutaja ugonjwa huo kuwa mafua tu yasiyokuwa na athari kubwa.

Rais Jair Bolsonaro alipimwa Jumatatu baada ya kuonesha dalili ikiwemo kiwango cha juu cha joto.

Aidha Bwana Bolsonaro pia alikuwa ametaka magavana kulegeza masharti yaliyokuwa yamewekwa kama njia moja ya kukabiliana na ugonjwa wa virusi vya corona akisema kwamba hatua hizo zimeathiri uchumi na Jumatatu alipuuzilia mbaya kanuni ya kuvaa barakoa.

Bwana Bolsonaro ametangaza hilo Jumatatu kupitia mahojiano kwa njia ya televisheni Jumanne.

Alisema kwamba joto ambalo amekuwa akihisi sasa hivi limeanza kurudi chini na kwamba amepata afueni kubwa.

Aprili, Bolsonaro aliwahi kusema kwamba hata akipata maambukizi ya virusi hivyo, hatakuwa na haja ya kuwa na wasiwasi wowote kwasababu zaidi itakuwa ni kama mafua tu au homa.

Alipokuwa anatoa tangazo hilo, idadi ya waliothibitishwa kufa kwa ugonjwa wa Covid-19 nchini humo ilikuwa bado ni chini ya 3,000 huku maambukizi yakiwa karibu 40,000.

Lakini idadi hiyo imekuwa ikiongezeka tangu wakati huo.

Kufikia Jumatatu, idadi ya waliokufa ilikuwa ni zaidi ya 65,000 huku maambukizi yakiwa zaidi ya milioni 1.6, ikiwa ya pili baada ya Marekani kwa nchi zilizoathirika vibaya na ugonjwa wa virusi vya corona.

Licha ya idadi hiyo kuzidi kuongezeka, rais Bolsonaro amekuwa akisema kuwa athari za kufungwa kwa maeneo ni kubwa mno kuliko za virusi vyenyewe na kushtumu vyombo vya habari kwa kusababisha hofu miongoni mwa raia.

Wakati anatoa cheche za maneno namna hiyo mwezi wa Machi, amekuwa akienda kinyume na hatua zilizowekwa za kukabiliana na virusi vya corona alizozichukulia kama udikteta mfano kufunga maeneo ya ufukweni au kuvaa barakoa.

Jumatatu, alifanya mabadiliko zaidi ya sheria ambayo yangetaka raia wa Brazil kuvaa barakoa wakiwa maeneo ya umma.

Pia, Bolsonaro amehudhuria matukio kadhaa ya umma bila kuvaa barakoa hata wakati ambapo alihitajika kuvaa.

Jumapili, Waziri wa Mambo ya Nje Ernesto Araújo alituma picha mtandaoni inayomuonesha yeye na Rais Bolsonaro pamoja na wengine wakihudhuria 'Sikukuu ya Uhuru' katika ubalozi wa Marekani nchini Brazili.

Hakuna kati ya picha hizo iliyomuonesha Bolsonaro amevaa barakoa au anafuatilia hatua ya kutokaribiana.

Ubalozi wa Marekani ulisema kwamba balozi wa Marekani amekula chakula cha mchana na Bwana Bolsonaro pamoja na wengine Julai 4.

Ubalozi uliongeza kwamba balozi huyo hakuwa na dalili zozote lakini hatahivyo, atafanyiwa vipimo.

Awali, balozi alikuwa ametuma kwenye mtandao wa Twitter picha yake yeye na Rais Bolsonaro.