Rambirambi zazidi kutumwa kufuatia kifo cha muigizaji Papa Shirandula

Risala za rambirambi zinaendelea kutumwa mitandaoni kufuatia kifo cha mcheshi Charles Bukeko almaarufu Papa Shirandula, aliyefariki jana hospitalini jijini Nairobi.

Inaarifiwa kuwa muigizaji huyo alipatwa na matatizo ya kupumua na kupelekwa hospitalini lakini akafariki muda mfupi baadae. Amewacha mke na watoto watatu.

Huzuni imetanda katika mtaa wa Burumba C mjini Busia kufuatia kifo cha staa huyo. Ndunguye marehemu Nick Wafula anasema kama familia wamepokea ripoti ya kifo chake kwa mshangao na masikitiko makubwa. Mashabiki wake nao wamemuomboleza wakisema wataukosa ucheshi na mafunzo ambayo Papa Shirandula alikuwa anawatumbuiza nayo kwa kipindi chake.

Hayo yakijiri, baadhi ya makanisa yanafunguliwa hii leo kwa ibada ya jumapili, na kutii kanuni kali zilizowekwa ikiwemo kuwa na waumini 100 tu kwa kila ibada, huku ibada zikitakiwa kudumu kwa saa moja pekee. Baadhi ya viongozi wa kanisa wanasema watawasajili waumini mlangoni ili kuthibiti idadi ya waumini wanaohudhuria ibada.

Baadhi ya viongozi wa makanisa sasa wanadai kuwa ni vigumu kwao kufanya idaba mirandaoni kama wenzao, kwani waumini wao hawawezi kusikia huduma za mitandanao. Wanasema ingawaje kanuni zilizowekwa ni kali, itawabidi kutii kwa ajili ya usalama wa waumini wao, lakini wanataka baadhi ya kanuni hizo kupitiwa upya.

Kwinginelo, vijana mumeshauriwa kujiepusha na uraibu wenye madhara, wakati huu ambapo masomo yamekatizwa. Katibu katika wizara ya elimu ya vyuo vikuu Simon Nabukwesi anasema uhalifu na utumizi wa mihadarati ni mojawapo ya mambo ambayo vijana wanajihusisha nayo kwa kuwa hawana la kufanya.