Real Madrid imetupilia mbali nia yao ya kumsajili mshambulizi Neymar Jr

neymar
neymar
Real Madrid imetupilia mbali nia yao ya kumsajili mshambulizi  Neymar Junior, kutoka PSG. Miamba hao wa Uhispania walikua wanamtaka mchezaji huyo huku raisi wa klabu Florentino Perez akidai kumleta ugani  Bernabeu.

Hata hivyo Madrid wamejiondoa katika mbio za kumsajili kwani mahasimu wao Barceona pia wanamdai. Kulingana na ripoti kutoka Uhispania, Los blancos badala yake wanataka kumsajili Kylian Mbappe kutoka PSG.

Barcelona inakaribia kumsajili mshambuliaji wa Ufaransa na Atletico Madrid Antoine Griezmann kutoka Atletico Madrid kwa dau la pauni milioni 107.

Duru kutoka Barcelona zimekana ripoti kwamba tayari klabu hiyo imetoa dau hilo. Kwingineko Mshambuliaji Gareth Bale mwenye umri wa miaka 29, alishiriki mazoezi na wenzake wa Real Madrid nchini Canada huku akiendelea kujilazimisha katika mipango ya mkufunzi Zinedine Zidane.

Huko Uingereza, Newcastle inajiandaa kumteua mkufunzi wa Sheffield Wednesday Steve Bruce kuwa kocha wake na wanatumai ataweza kujiunga na timu hiyo katika maandalizi ya msimu ujao wakiwa ziarani nchini Uchina.

Newcastle pia inajadiliana kuhusu fidia ya takriban pauni milioni 5 na klabu hiyo ili kumsajili Bruce.

Vilabu vinavyoshiriki Ligi ya mabingwa, Ligi ya Uropa na Uefa Super Cup msimu huu watapokea mgao wa pauni bilioni 2.9.

Kiwango hicho hakijabadilika kutoka kile vilabu walipokea msimu uliopita. Shirikisho la soka la Uropa Uefa linasema milioni 470 zitatolewa kulipia gharama ya maandalizi na malipo ya pamoja.

Wakati huo huo vilabu vitakavyoshiriki ligi ya Uropa msimu ujao vitapokea mgao wa pauni milioni 503. Mabingwa wa Champions League Liverpool watapambana na mabingwa wa Ligi ya Uropa Chelsea katika Uefa Super Cup huko Uturuki mwezi Agosti.

Tukirejea Afrika, Bandari watapambana na mabingwa watetezi Azam leo jioni katika mechi yao ya mwisho ya makundi katika kombe la Cecafa Kagame Cup nchini Rwanda, huku wakiwania kufika katika robo fainali.

Mabingwa hao wa kombe la FKF  walitoka sare  ya 1-1 na  KCCA ya Uganda kabla ya kupiga sare nyingine ya 2-2 dhidi ya wenyeji Mukura Victory. Mabingwa wa KPL Gor Mahia tayari wamefuzu kwa robo fainali, huku wakiwa na mechi mmoja mkononi dhidi ya KM ya Zanzibari wikendi hii.