Robert Alai apondwa mtandaoni baada ya DCI kumwanika na picha ya ‘mhalifu’

Robert Alai
Robert Alai
Mwanablogu Robert Alai ndiye hujipata akiwafanyia watu kejeli mtandaoni kupitia  maoni yake ambayo  wakati mwingine huwa ya kikatili . Lakini leo amejipata amevalia kiatu tofauti cha kufanyiwa kejeli hizo na wakenya mtandaoni baada ya idara ya DCI kutoa picha yake  akiwa amebeba bango lenye  maelezo yake baada ya kukamatwa kwa kueneza mtandaoni picha za miili ya polisi waliouawa huo wajir katika shambulizi la kigaidi .

Alai amejipata matatani baada ya tume ya Uwiano na maridhiano kutangulia kumsihi aziondoe picha hizo katika mitandao ya kijamii lakini akapuuza . Katika kinachothibitisha msemo aliye juu mngoje chini ,Alai hajaonewa huruma na wengi wanaomponda huku wengine wakimrejesha nyuma kumkumbusha kuhusu ukosoaji wake mkali dhidi ya kinara wa ODM  Raila Odinga .

Hata hivyo baadhi ya wanamtandao hawajapendezwa na hatua ya polisi kuiweka nambari ya simu ya Alai hadharani katika kibango alichopigwa nacho picha .