Robert Mugabe: Uhuru Kenyatta atuma risala za rambi rambi

mugabe
mugabe

Kwa niaba ya Serikali, na Watu wa Jamhuri ya Kenya na kwa niaba yangu binafsi, ningependa kutoa pole na risala za rambi rambi kwa Serikali na watu wa Jamhuri ya Zimbabwe kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Robert Gabriel Mugabe.

Kwa wakati huu wa majonzi, mawazo na maombi yangu ni kwa jamaa, ndugu na watu wa Zimbabwe ambao kwa miaka mingi aliwatumikia kwa kujitolea na kwa bidii.

Sina maneno ya kutosha kuelezea  uzito wa  kuachwa na  kiongozi shupavu, shujaa na mzalendo wa Afrika ambaye alitekeleza jukumu muhimu katika kutetea maslahi ya bara la Afrika

Bila shaka, tutamkumbuka Rais huyo wa zamani Robert Mugabe kama mtu jasiri ambaye kamwe hakuogopa kuelezea msimamo wake kwa jambo lolote hata kama wengi hawakumuunga mkono.

Kwa familia yake, Serikali na raia wa Zimbabwe, Mola awafariji na ailaze roho ya Rais wa zamani Robert Mugabe mahala pema peponi.