‘Rogue Station’: Kayole Police, Kitovu cha maovu, wizi na mauaji ya kiholela

Ahadi inayotolewa na huduma ya polisi nchini Kenya ni ‘utumishi kwa wote ‘ na unatarajia kwamba kuna  utu ,kujitolea, uaminifu na uadilifu katika utendakazi  miongoni mwa polisi wa humu nchini .

Licha ya juhudi za kujaribu kuipa sura mpya huduma ya polisi na kuifanya iweze kuaminiwa na umma, huduma ya polisi nchini imezidi kujipata pabaya machoni mwa umma kwa kufuatia mienendo ya baadhi ya maafisa wake wasiotii sheria au kujali haki za kimsingi za binadamu. Kando na visa vya hivi karibuni tangu kutangazwa kwa marufuku ya kutotoka nje na kusababisha  baadhi ya polisi kuwapa kipigo raia na hata kumuua mtoto wa miaka 13 katika mtaa kiamaiko, utovu wa nidhamu kwa upande wa polisi ni tatizo ambalo limekuwepo kwa muda mrefu sana.

Iwapo kuna kituo cha polisi humu nchini ambacho kimechangia  pakubwa kuwaharibia polisi sifa na  utendakazi wao , basi kituo cha polisi cha Kayole, jijini Nairobi hakiwezi kusahaulika.  Kwa sasa kituo hicho na maafisa wanaohudumu hapo wametajwa pakubwa kuhusiana na mauaji ya mshukiwa wa ujambazi aliyehusishwa  na  wizi wa shilingi milioni 72  katika mashine moja ya ATM Nairobi West, Wycliffe Vincent Owuor ambaye kifo chake wiki jana kimezua maswali kuliko majibu kwani ripoti za hali iliyosababisha kifo chake zinakinzana. Polisi wanasema  aliuawa katika ufyatilianaji wa risasi   na maafisa wa usalama lakini wakili wake Cliff Ombetta  amedai kwamba mteja wake aliauawa kinyama.

Kabla ya  kuibuka ripoti za uhusiano wa karibu kati ya  Owuor na baadhi ya maafisa katika kituo hicho, kumekuwa na msururu wa maafisa wa polisi wa kituo hicho waliojipata  katika mkondo mbaya wa sheria  baada ya kuhusishwa na wizi wa kimabavu na mauaji ya kiholela   na kituo hicho kinachunguzwa kwa visa kama hivyo.

Mmoja wa waathiriwa Daniel Wang’ombe  alifariki  Disemba tarehe 19 katika kituo hicho katika hali ya kutatanisha .Mwingine Magdaline Ombango  alikamatwa na kuzuiliwa kituoni humo lakini akaaga dunia akiwa seli baada ya kudaiwa kuanguka . Mwaka uliopita  maafisa wawili wa polisi kutoka kituo hicho  walikamatwa kwa   kuwa sehemu ya genge la majambazi waliomwibia mfanyibiashara mmoja wa eastleigh shilingi milioni 6 . Mmoja wa maafisa hao  Simon Mwaniki baadaye alishtakiwa katika  mahakama ya makadara kwa wizi huo .

Mwaniki pia alishtakiwa kwa wizi wa kimabavu  baada ya kuhusishwa katika genge lililoiba shilingi milioni 2.7 kutoka kwa  mwekezaji mmoja Wuwei Dun  ambaye  alikuwa kielekea Nakuru na wafanyikazi wake wawili na gari lao kusimamishwa na watu waliokuwa wamejihami  akiwemo afisa huyo wa polisi. Kando na visa hivyo, Mamlaka ya Ipoa  na kitengo cha kushughulikia lalama ndani ya Huduma ya polisi kinawachunguza polisi kadhaa kituoni humo kwa maovu mbalimbali .